BENKI Kuu ya Tanzania inapenda
kuufahamisha Umma kuhusu zoezi la kuondoa kwenye mzunguko noti za zamani za
shilingi ishirini (20), mia mbili (200), mia tano (500), elfu moja (1000), elfu
mbili (2000), elfu tano (5000) na elfu kumi (10000) kwa matoleo ya mwaka 1985
hadi mwaka 2003, na noti ya shilingi mia tano (500) iliyotolewa mwaka 2010
zenye sifa zilizoainishwa kwenye Tangazo la Serikali Na. 858 la tarehe 11
Oktoba 2024.
Zoezi la ubadilishwaji linatarajiwa kuanza tarehe 06 Januari 2025 hadi
tarehe 05 Aprili 2025 kupitia Ofisi zote za Benki Kuu na benki zote za biashara
kwa kupatiwa malipo yenye thamani sawasawa na kiasi kitakachowasilishwa. Aidha,
matumizi ya noti hizo yatafikia ukomo wa kuwa fedha halali za Tanzania kuanzia
tarehe 06 Aprili, 2025. Baada ya tarehe hiyo, mtu yeyote au taasisi yoyote
inayomiliki fedha hizo haitaruhusiwa kuzitumia katika kufanya malipo popote
duniani; na benki zote hazitaruhusiwa kulipa wala kupokea amana au maombi ya
kubadilisha noti zilizoondolewa kwenye mzunguko.
Hivyo, Benki Kuu inatoa rai kwa wananchi wote wenye akiba ya noti hizo za
zamani, kuzibadilisha au kuziweka amana kwenye benki yoyote ndani ya kipindi
kilichotolewa.
Kwa taarifa au msaada zaidi tafadhali wasiliana na: Kurugenzi ya Usimamizi wa
Sarafu, Benki Kuu ya Tanzania, 2 Mtaa wa Mirambo, S.L.P 2939 Dar es Salaam; au
kwa Barua Pepe: info@bot.go.tz au botcommunications@bot.go.tz; au kwa simu +255
745 802 007.
No comments:
Post a Comment