𝐌𝐁𝐖𝐀𝐌𝐁𝐎 𝐀𝐙𝐈𝐍𝐃𝐔𝐀 𝐉𝐔𝐊𝐖𝐀𝐀 𝐋𝐀 𝐖𝐀𝐍𝐀𝐖𝐀𝐊𝐄 𝐌𝐀𝐊𝐔𝐁𝐔𝐑𝐈, 𝐀𝐇𝐀𝐌𝐀𝐒𝐈𝐒𝐇𝐀 𝐔𝐖𝐄𝐙𝐄𝐒𝐇𝐀𝐉𝐈 𝐖𝐀 𝐊𝐈𝐔𝐂𝐇𝐔𝐌𝐈 - UMOJA BANKING BLOG

Breaking

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, 26 April 2026

𝐌𝐁𝐖𝐀𝐌𝐁𝐎 𝐀𝐙𝐈𝐍𝐃𝐔𝐀 𝐉𝐔𝐊𝐖𝐀𝐀 𝐋𝐀 𝐖𝐀𝐍𝐀𝐖𝐀𝐊𝐄 𝐌𝐀𝐊𝐔𝐁𝐔𝐑𝐈, 𝐀𝐇𝐀𝐌𝐀𝐒𝐈𝐒𝐇𝐀 𝐔𝐖𝐄𝐙𝐄𝐒𝐇𝐀𝐉𝐈 𝐖𝐀 𝐊𝐈𝐔𝐂𝐇𝐔𝐌𝐈

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoa wa Dar es Salaam, Ndg. Mwajabu Rajabu Mbwambo, amezindua rasmi Jukwaa la Wanawake katika Kata ya Makuburi, Wilaya ya Ubungo, ikiwa ni hatua muhimu katika kuwaunganisha wanawake na vijana kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Uzinduzi huo umefanyika katika kongamano maalum lililojulikana kama Makuburi Gala, ambapo jukwaa hilo limewakutanisha wajasiriamali kutoka makundi mbalimbali, wakiwemo wafanyabiashara, wanasiasa, wanamichezo pamoja na vijana.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mbwambo amewahimiza wanawake kusimama imara kiuchumi, huku wakitambua na kutekeleza wajibu wao wa msingi katika malezi bora ya watoto na familia kwa ujumla.

Mwambo ameeleza kuwa malezi yenye maadili na nidhamu ni msingi wa kujenga taifa lenye wananchi wanaojitambua na kuwajibika

Amewakumbusha wanawake umuhimu wa kutunza afya zao, pamoja na kuchukua tahadhari katika malezi ya watoto, hasa kwa kudhibiti matumizi ya simu janja na mitandao ya kijamii ili kuwaepusha na athari za uraibu wa kidijitali.

Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Kulwa Gumbo, Mwenyekiti wa UWT Kata ya Makuburi , Editha Ngotanile pamoja na Katibu Severina Minga, wamesisitiza dhamira ya jukwaa hilo kuwa chachu ya maendeleo na uwezeshaji wa wanawake katika sekta mbalimbali.

Ushiriki huo umeelezwa kuchangia kuimarisha upendo, umoja, mshikamano na amani ndani ya jamii.

Uzinduzi wa jukwaa hilo uliambatana na shughuli ya harambee iliyolenga kuchangisha fedha kwa ajili ya kuongeza mtaji na rasilimali za jukwaa. Pia zawadi zilitolewa kwa washiriki walioshinda katika bonanza la michezo ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha ushiriki na kuendeleza vipaji.

Katika uzinduzi huo viongozi mbalimbali wameshiriki wakiwemo viongozi wa UWT Wilaya ya Ubungo, pamoja na viongozi wa serikali na chama katika ngazi ya kata, jambo lililoonyesha mshikamano wa kiuongozi katika kuunga mkono jitihada hizo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad

Pages