Na Mwandishi Wetu
Kampuni ya
Taifa Gas imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi na salama
ya gesi, sambamba na kuhamasisha usalama mahali pa kazi katika maadhimisho ya
Wiki ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani.
Akizungumza katika viwanja vya Shule ya Msingi Mji Mwema, Njombe,
Mtaalamu wa Masuala ya Afya, Mazingira, Usalama na Ulinzi Mahali pa Kazi kutoka
Taifa Gas, Aurelius Marcus Mdemu, alisema kampuni hiyo imeshiriki maadhimisho
hayo yanayoanza Aprili 24 hadi 29, 2026 kwa lengo la kutoa elimu kwa wateja na
jamii kwa ujumla.
Alisema kupitia banda lao, wanaonesha vifaa mbalimbali vinavyotumika
kazini ili kuimarisha usalama wa wafanyakazi, pamoja na kutoa elimu kuhusu
matumizi sahihi ya gesi na faida zake. Aidha, alieleza kuwa wanajitahidi
kuondoa hofu na dhana potofu zilizopo miongoni mwa watumiaji wa gesi.
“Tunawaonesha wananchi namna Taifa Gas
inavyoweka kipaumbele kwenye usalama wa wafanyakazi, ikiwa ni pamoja na
matumizi ya vifaa kinga vinavyotakiwa kutumika muda wote wakiwa kazini,”
alisema Mdemu.
Kwa upande wake, Afisa Masoko wa Chapa wa Taifa Gas, Santina Ngaponda,
alisema maonyesho hayo yameandaliwa na OSHA, yalianza Aprili 24 na yanatarajiwa
kufikia kilele chake Aprili 29 mwaka huu.
Ngaponda aliwahimiza wakazi wa Njombe na maeneo
ya jirani kutembelea banda la Taifa Gas ili kupata elimu kutoka kwa wataalamu
wa usalama, kujifunza matumizi sahihi ya gesi, pamoja na kuona vifaa vya
usalama vinavyotumika kazini na umuhimu wake.
Aidha, aliongeza kuwa kampuni hiyo inatoa punguzo maalum la bei ya gesi
na vifaa vyake, pamoja na zawadi mbalimbali kwa wateja watakaotembelea banda
hilo.
Naye Meneja Mauzo wa Kanda ya Nyasa wa Taifa Gas, Arnold Salewa, alisema
wanaendelea kutumia maonyesho hayo kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya
nishati safi pamoja na kuuza bidhaa zao kwa bei ya promosheni.
Alisema kanda hiyo inajumuisha mikoa ya Njombe,
Iringa na Ruvuma, na kwamba pia wanatoa fursa kwa wananchi wanaotaka kuwa
mawakala wao, kwa kuwapatia elimu ya biashara na usimamizi salama wa mitungi ya
gesi.
Salewa alisisitiza kuwa Taifa Gas ipo mstari wa mbele kuhakikisha kaya,
migahawa na taasisi mbalimbali zinaanza kutumia nishati safi ya kupikia kwa
gharama nafuu, ili kupunguza athari za matumizi ya mkaa na kuni kwa mazingira
na afya za Watanzania.
Aliongeza kuwa mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa, huku Taifa Gas ikiendelea kuwa chaguo sahihi kwa watumiaji wengi nchini.




No comments:
Post a Comment