NHC YASHIRIKIANA NA BENKI TISA KUPANUA FURSA ZA MIKOPO YA NYUMBA KWA WATANZANIA - UMOJA BANKING BLOG

Breaking

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, 19 October 2026

NHC YASHIRIKIANA NA BENKI TISA KUPANUA FURSA ZA MIKOPO YA NYUMBA KWA WATANZANIA

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw. Hamad Abdallah, akizungumza na wateja, wadau wa benki na taasisi za fedha pamoja na wadau wengine wakati wa kilele cha Wiki ya Huduma kwa Wateja kilichofanyika Oktoba 16, 2026, katika mradi wa Kawe 711, Dar es Salaam.

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeimarisha ushirikiano na benki na taasisi tisa za fedha ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo ya nyumba kwa Watanzania, wakiwemo wanaoishi nje ya nchi, kwa lengo la kuongeza fursa za kumiliki makazi bora na ya kisasa.


Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw. Hamad Abdallah, amesema ushirikiano kati ya Shirika hilo na taasisi za fedha ni nyenzo muhimu katika kutimiza dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kumiliki nyumba bora.


Akizungumza katika kilele cha Wiki ya Huduma kwa Wateja kilichofanyika Oktoba 16, 2026, katika mradi wa Kawe 711, Dar es Salaam, Bw. Abdallah amesema NHC inaendelea kuimarisha ushirikiano na benki mbalimbali ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo ya nyumba kwa wananchi, wakiwemo Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora).


“Tunataka kutimiza ndoto ya Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kumiliki nyumba. Hili linawezekana kupitia ushirikiano na mabenki yanayotoa mikopo kwa Watanzania waliopo nchini na wanaoishi nje ya nchi,” amesema.

Meneja wa Mauzo na Masoko wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw. Deogratius Batakanwa, akibadilishana mawazo na wadau wa Shirika hilo.

Katika hafla hiyo, benki na taasisi tisa za fedha zilishiriki kutoa elimu kuhusu fursa mbalimbali za mikopo ya nyumba kwa wafanyakazi, wafanyabiashara, wawekezaji na Watanzania wanaoishi nje ya nchi.


Taasisi hizo ni CRDB Bank, NMB Bank, NBC Bank, Azania Bank, Absa Bank, Equity Bank, Bank of Africa Tanzania, Tanzania Commercial Bank (TCB) na First Housing Finance.

Wadau kutoka Azania Bank wakijadiliana na wateja wao wakati wa kilele cha Wiki ya Huduma kwa Wateja.

Bw. Abdallah amesema lengo la kuzikutanisha taasisi hizo za fedha na wananchi ni kuwawezesha wateja kupata taarifa za mikopo moja kwa moja kutoka kwa wataalamu wa fedha, kulinganisha masharti ya ukopeshaji na kufanya maamuzi sahihi kuhusu umiliki wa nyumba.


Azania Bank Yatoa Mikopo ya Nyumba ya Hadi Miaka 25

Akizungumza kwa niaba ya Azania Bank, Bw. Samson Mhindi amesema benki hiyo imekuwa na ushirikiano na NHC kwa takribani miaka 15, ambapo imewawezesha Watanzania wengi kumiliki nyumba katika miradi mbalimbali, ikiwemo Kawe na Iyumbu, Dodoma.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw. Hamad Abdallah, akijadiliana jambo na wadau kutoka CRDB Bank.

Amesema Azania Bank inatoa mikopo ya nyumba yenye muda wa marejesho unaofikia miaka 25. Aidha, baadhi ya miradi ina utaratibu maalumu wa riba ya asilimia tisa, hatua inayolenga kupunguza mzigo wa marejesho kwa wanunuzi wa nyumba.


Kwa upande wake, mwakilishi wa Equity Bank amesema benki hiyo ina ushirikiano wa muda mrefu na NHC na uzoefu katika utoaji wa mikopo ya nyumba. Ameeleza kuwa benki hiyo inaweza kutoa mkopo unaofikia Shilingi bilioni 3.5 kwa mkopaji mmoja, kutegemea vigezo na tathmini ya uwezo wa mkopaji.

Naye Meneja wa Mikopo ya Nyumba wa TCB, Bi. Maria Mbuta, amesema benki hiyo inatoa mikopo inayozingatia mahitaji na uwezo wa kifedha wa mteja, ikiwemo mikopo ya kununua, kujenga na kukarabati nyumba.


Kwa upande wa Absa Bank Tanzania, Bi. Sylvia Abraham amesema benki hiyo inaweza kufadhili hadi asilimia 90 ya bei ya nyumba, kwa mkopo unaofikia Shilingi bilioni moja, huku pia ikitoa huduma maalumu za kifedha kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi.


Mwakilishi wa First Housing Finance, Bi. Fausta Arnold, amesema taasisi hiyo imejikita katika kutoa mikopo ya nyumba kwa wafanyakazi na wafanyabiashara, yenye muda wa marejesho unaofikia miaka 20.


Ameipongeza NHC kwa kuendeleza miradi ya nyumba zenye ubora na kuwahimiza wananchi kutumia fursa za mikopo zinazopatikana ili kutimiza ndoto zao za kumiliki makazi.


Wawakilishi wa CRDB Bank, NMB Bank, NBC Bank na Bank of Africa Tanzania pia walishiriki kuhamasisha wananchi kutumia huduma za mikopo ya nyumba. NMB Bank ilieleza kuwa ina utaratibu wa marejesho unaoweza kuzingatia mzunguko wa mapato ya mteja.


Mwekezaji Ahamasisha Watanzania Kuwekeza katika Nyumba

Katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kezmak Inc., Bw. Mabrouk Ambali, ambaye pia ni mteja aliyenunua nyumba kupitia NHC, amewahamasisha Watanzania kuwekeza katika sekta ya nyumba, akieleza kuwa umiliki wa nyumba ni fursa ya kujenga utajiri na kuongeza kipato kupitia upangishaji.


Amesema nyumba inaweza kutumika kwa makazi binafsi au kupangishwa ili kumwingizia mmiliki kipato cha ziada, hata akiwa ameajiriwa au anaishi nje ya nchi.


Ameipongeza NHC kwa kuendeleza miradi yenye ubora na kuwataka Watanzania kutumia fursa zilizopo kuwekeza katika sekta ya milki, badala ya kusubiri hadi wawe na fedha zote za kununua nyumba.


Kawe 711: Makazi ya Kisasa Yenye Fursa za Uwekezaji

Akizungumzia mradi wa Kawe 711, Bw. Abdallah amesema mradi huo una nyumba 122 zilizojengwa kwa kuzingatia mahitaji ya maisha ya kisasa.


Amesema nyumba hizo zinaungwa mkono na huduma muhimu, zikiwemo mifumo ya kuhifadhi maji, majenereta ya dharura, viwanja vya michezo na bwawa la kuogelea.


Ameongeza kuwa mradi huo upo takribani mita 50 kutoka Bahari ya Hindi, jambo linaloongeza mvuto wa eneo hilo na uwezekano wa kuongezeka kwa thamani ya nyumba katika siku zijazo.


“Kuna kumiliki nyumba, lakini kuna kumiliki nyumba katika eneo zuri. Thamani ya nyumba inategemea eneo ilipo, eneo ilipo na eneo ilipo,” amesisitiza.

 

Amesema NHC itaendelea kuendeleza miradi ya nyumba katika maeneo yenye miundombinu na mazingira bora, huku ikiimarisha ushirikiano na taasisi za fedha ili kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata fursa za kumiliki nyumba.


Kwa mujibu wa Bw. Abdallah, ushiriki wa taasisi hizo tisa za fedha katika kilele cha Wiki ya Huduma kwa Wateja umeonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya NHC na sekta ya fedha katika kupanua fursa za umiliki wa nyumba na uwekezaji nchini.


Kupitia ushirikiano huo, wananchi wanapata fursa ya kupata taarifa na kulinganisha huduma za mikopo zinazolingana na mahitaji na uwezo wao wa kifedha, huku NHC ikiendelea kutekeleza dhamira yake ya kuongeza upatikanaji wa makazi bora kwa Watanzania.


“Huna fedha zote za kununua nyumba? Haimaanishi huwezi kumiliki nyumba. Fursa za mikopo zipo, chukua hatua kutimiza ndoto yako!” amesisitiza.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad

Pages