Waziri Mohamed Mchengerwa.
...............................................
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa , Mhe.Mohamed
Mchengerwa amesema Mkuu wa Mkoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali
za Mitaa watakaobainika maeneo yao kuwa na vikundi hewa kwenye mikopo kwa
vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu watawajibishwa.
Aidha, zaidi ya Sh.Bilioni 234 zinakusudiwa kupelekwa kwa wananchi kwa njia
mbili za utoaji mikopo hiyo ambazo ni kupitia Benki kwa Halmashauri 10 na
mikopo iliyoboreshwa kwenye Halmashauri 174.
Akizungumza Februari 7, 2025 jijini Dodoma kwenye hafla ya utiaji saini
mikataba kati ya Halmashauri 10 na Benki tatu ya utoaji mikopo hiyo inayotokana
na asilimia 10 ya mapato ya ndani, Mhe. Mchengerwa amesema kila mmoja afuatilie
fedha hizo kuhakikisha zikishuka kama ilivyokusudiwa kwa walengwa ili
zitabadili maisha yao.
Amesisitiza uadilifu wa kwenye fedha hizo na kufuatilia kwa kina vikundi vyote
na kuvijua na asisikie vikundi hewa.
“Fedha hizi ni za moto wajibu wetu ni kumsaidia Rais fedha hizi zisiende
kuchezewa, naelekeza kikundi hewa kitakachobainika eneo lolote viongozi wa eneo
hilo mtapaswa kuwajibika, tumieni vyombo mnavyosimamia kwenye mikoa na wilaya
kuhakikisha hakuna vikundi hewa, fedha zisimamiwe na kurejeshwa.”
“Nazielekeza Mamlaka za serikali za mitaa kuendelea kuchangia fedha za mapato
ya ndani kwa ajili ya mikopo hii kwa mujibu wa sheria ya fedha za serikali za
mitaa, na Katibu Mkuu niletee orodha kama kuna halmashauri ambazo hazijachangia
na zinadorora kuchangia na kama kuna halmashauri ambayo haijatekeleza maelekezo
ya Rais,”amesema.
Amesema Benki ya NMB itafanya kazi kwenye halmashauri za wilaya za Bumbuli,
Itilima, Newala, Manispaa ya Songea, Jiji la Dodoma na Jiji la Dar es salaam
huku benki ya CRDB itafanya kazi Wilaya za Nkasi, Mji wa Mbulu, Manispaa ya
Kigoma, Jiji la Dodoma na Jiji la Dar es salaam na Benki ya Biashara ya Uchumi
itafanya kazi Halmashauri ya Wilaya ya Siha.
Awali, Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Adolf Ndunguru amesema kusainiwa mikataba hiyo
ni mwanzo wa mapinduzi ya kuhakikisha mikopo hiyo ya asilimia 10 inakuwa na
tija tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
No comments:
Post a Comment