SERIKALI imeipongeza Benki ya NMB kwa kuzindua Mfuko Maalum
uliotengewa Sh. Bilioni 100 za kukopesha wasambazaji na wauzaji wa Nishati Safi
ya Kupikia kwa Watanzania, na kwamba Serikali itaingia kifua mbele katika
Mkutano Mkuu wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika (Mission 300), unaofanyika
Januari 27 na 28 jijini Dar es Salaam.
Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Waziri Mkuu, Dk. Doto Biteko,
wakati wa uzinduzi wa mfuko huo, aliobeba dhamira chanya ya kuunga mkono juhudi
za Serikali katika Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia
(2024-2034) na kwamba tukio hilo ni uthibitisho tosha wa ushirikiano uliopo
baina ya Serikali na Sekta Binafsi katika kustawisha jamii ya Watanzania.
Kwa niaba ya Serikali na Wizara ya Nishati, Dk. Biteko aliishukuru
NMB kwa wazo hili na kwamba wako tayari kuwaunga mkono ili jambo hilo
likatimizwe, huku akisema wazo la kuhakikisha mawakala na wasambazaji wa
nishati safi za kupikia wanapata mitaji ili kufikisha huduma mijini na
vijijini, litasaidia kuchochea upatikanaji na matumizi ya nishati hiyo.
“Hakika mpango huu wa NMB kutenga Shilingi Bilioni 100 kwa ajili
ya jambo hili, unastahili pongezi kubwa sana, hasa ikizingatiwa kuwa kama benki
ina njia nyingi sana za biashara, ambazo wangeweza kuwekeza fedha hizo sehemu
nyingine ili kuweza kuendelea kujizalishia faida zaidi.
“Lakini, msukumo huu wa kuja kuweka kiasi hiki kwenye Nishati Safi
ya Kupikia inaonesha dhamira ya dhati ya benki kuchangia maendeleo endelevu kwa
taifa letu la Tanzania, lakini ni kielelezo tosha cha uzalendo wa kweli uliopo
kati yenu Menejimenti pamoja na wafanyakazi wa benki hii.
“Mtendaji Mkuu wa NMB tayari ameeleza hapa faida mbalimbali za
matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na mimi nisisitize kuwa, faida hizo za Afya
Bora, Mazingira Safi, Kuboresha Uchumi na Ufanisi wa Nishati hizi na ukweli
kuwa nishati safi ni salama, ndio maana hata Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa
kinara wa hili nchini, Afrika na duniani kote.
“Wote tunafahamu kwamba, licha ya ukosefu wa mitaji, changamoto
kubwa ya wananchi kuendelea kutumia nishati isiyo safi ya kupikia, ni ukosefu
wa elimu juu ya nishati safi ya kupikia, hivyo suala la NMB kuanza pia kutoa
elimu ya hili ni jambo zuri na la kipekee sana kwa ustawi wa matumizi ya
nishati hii safi.” Alisema Dk. Biteko.
Alibainisha kuiwa shukrani na pongezi kwa NMB hazitaishia tu
katika Nishati Safi ya Kupikia tu, bali zinaenda pia kwa mambo makubwa ambayo
imekuwa ikifanya kwa manufaa kwa taifa letu la Tanzania, ikiwemo misaada
mbalimbali mashuleni, zahanati, vituo vya afya na hospitali na kuchagiza maendeleo
endelevu kwa jamii, sambamba na upandaji miti.
Januari 27 na 28, Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa mkutano
uliopewa jina la Mission 300 kuakisi dhamira ya kuwafikia watu milioni 300
barani Afrika kuhakikisha wanatumia Nishati Safi, ambapo zaidi ya marais 25,
Mawaziri wa Fedha na Nishati 60 wa Afrika, watashiriki mkutano huo, mweji akiwa
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Kwa kutambua umuhimu wa Mkutano huo na kuunga mkono juhudi za
Serikali ya Tanzania kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya
Kupikia, NMB inaamini kiasi ilichotenga kwa ajili kukopesha wadau wa biashara
ya Nishati Safi, utakuwa na mchango chanya kwa Taifa katika azma yake ya kukuza
kiwango cha matumizi ya nishati hiyo mjini na vijijini.
Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna, alisema
msukumo wa benki yake kutenga kiasi hicho kikubwa cha pesa za kukopesha
wafanyabiashara na wasambazaji wa nishati, unalenga kuwezesha utunzaji wa
mazingira, kuboresha afya na ustawi wa jamii, kukuza uchumi na kuchangia
kufikiwa kwa Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa ya Mwaka 2030.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Bi. Zaipuna alisema lengo ni
kuongeza urahisi katika upatikanaji wa nishati safi kwa Watanzania na kwamba,
NMB inatambua umuhimu wa kuungana na Serikali kufanikisha Mkakati wa Taifa wa
Matumizi ya Nishati Safi, wenye lengo la kuhakikisha upatikanaji wa nishati
nafuu, kwa urahisi, endelevu na ya kisasa kwa wote.
“Kama ulivyoainisha katika Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati
Safi ya Kupikia (2024-2034), ‘‘Umuhimu wa agenda hii kwa Taifa letu la
Tanzania, na dunia nzima kwa ujumla, unasukumwa na ongezeko la uharibifu wa
mazingira na mabadiliko ya tabianchi, pamoja na athari za kiafya zinazotokana
na matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia’’
“Takwimu zilizotolewa wakati wa Mkutano wa Clean Cooking
uliofanyika jijini Paris, Ufaransa, Mei, 2024, zinaonyesha kwa nini wadau wote
tunapaswa kushirikiana na Serikali, na Wananchi kukabiliana kwa haraka na suala
la ukosefu wa upatikanaji wa Nishati Safi ya kupikia barani Afrika.
“Takwimu hizo, ambazo ni za kushtusha, zinaonyesha kuwa, zaidi ya
watu Bilioni 1.2 barani Afrika hawatumii Nishati Safi za kupikia, na kuwalazimu
kutegemea mkaa na kuni kwa kupikia, hali inayochangia madhara makubwa ya
kiafya, kimazingira na kijamii na waathirika wakuu wa changamoto hii ni
wanawake, ambao ni dada zetu, na mama zetu, hasa wa vijijini.
“Matokeo yake, Afrika inapoteza zaidi ya wanawake na watoto
600,000 kila mwaka kutokana na athari za moshi wa utokanao na nishati chafu, na
Tanzania, kama ilivyoanishwa na Afisa Nishati Mkuu kutoka Wizara ya Nishati,
Mussa Abbas, zaidi wa watu 33,000 hufariki Tanzania kila mwaka kwa athari za
Nishati Chafu,” alisema Bi. Zaipuna.
Alibainisha kuwa, kiwango cha mwisho kwa mkopaji mmoja ni Sh. Bil.
1, ambao utakuwa wa riba nafuu na rafiki ya asilimia 1 kwa mwezi (sawa na
asilimia 12 kwa mwaka) na kuwa walengwa wakuu wa mkopo huu utakaopatikana
kwenye matawi yote, ni wasambazaji na mawakala wa mitungi na majiko ya gesi
ambayo kwa sasa ndio nishati safi zaidi inayopatikana kwa urahisi.
Aidha, akimkaribisha Naibu Waziri Mkuu kuzungumza katika uzinduzi huo, Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, aliipongeza NMB kuunga mkono juhudi za Serikali kufanikisha malenpo endelevu ya kufikisha huduma ya nishati kote nchini na kwamba benki hiyo imefanya jitihada kubwa katika kuwapambania Watanzania, wakiwemo wafanyabiashara na wajasiriamali wanawake.
No comments:
Post a Comment