KAMPUNI YA DONTINO WATER REFILLING Co.LTD INAVYOCHAGIZA UPATIKANA WA MAJI SAFI NA SALAMA DAR ES SALAAM - UMOJA BANKING BLOG

Breaking

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, 30 March 2026

KAMPUNI YA DONTINO WATER REFILLING Co.LTD INAVYOCHAGIZA UPATIKANA WA MAJI SAFI NA SALAMA DAR ES SALAAM

Inamilikiwa na mzalendo wa kweli aliyeamua kurudi nyumbani kuwekeza

Michael Kapaya mmoja wa wanufaika wa ubunifu wa viosk vya maji safi na salama ulioazishwa na Mwekezaji Mhandisi Valentino Ngaiyamu anaye miliki Kampuni ya Dontino Water Refilling Co.Ltd   akiwa katika majukumu yake.

...............................

Na Waandishi Wetu, Dar es Salaam

      KATIKA baadhi ya maeneo ya jiji la Dar es Salaam, kupata maji safi ya kunywa kwa gharama nafuu ya Shilingi. 200 za kitanzania imekuwa kama miujiza  kutokana na maeneo mengi ya pembezoni kutofikiwa na  Mamlaka ya Maji Safi na  Taka Dar es  Salaam (DAWASA)

 

 Kukosekana au kutofikiwa na mamlaka husika kumechangia kwa kiasi kikubwa wananchi wa kipato cha chini kupata changamoto ya maji ya kunywa kutokana na maeneo yao kuwepo kwa maji ya chumvi.

 

Wananchi wanalazimika kutumia gharama kubwa ili kupata maji salama kwa matumizi ya kila siku.


Hata hivyo, hali hiyo sasa inaanza kubadilika kufuatia uwekezaji wa mabomba ya maji kupitia vituo maalum vya kuuza maji (Water Kiosks) ulioanzishwa na Mwekezaji Mhandisi Valentino Ngaiyamu. 


Ngaiyamu ni Mhandisi ambaye alikuwa akifanya shughuli zake nje ya nchi na kuamua kurudi nyumbani na kuanzisha kampuni ya  Dontino Water Refilling Co.Ltd ambayo imeleta tabasamu kwa wananchi wa Dar es Salaam. 


  Aidha, Ngaiyamu anasema kuwa changamoto ya vipato kwa wakazi wengi wa jiji la Dar es Salaam pamoja na mitindo ya maisha ya muda mwingi kuwa kwenye shughuli za kujipatia vipato vya kukidhi mahitaji ya maisha hawana hawapati nafasi ya kuchemsha maji ya kunywa. 

   

"Nilikuwa Dubai nikaona wanachukua maji ya bahari wanayachuja na kuyatibu yanakuwa safi na salama  kwa kunywa," alisema Ngaiyamu. 


 Alisema kitendo hicho kilimuongezea ushawishi na kuona anakila sababu ya kuanzisha uwekezaji kwa lengo la kupunguza changamoto ya maji ya kunywa safi na salama kwa wananchi wa kipato cha chini ambao wanaishi chini ya Shilingi 5000 za kitanzania kwa siku wapate nafuu ya kupata bidhaa hiyo ambayo ni muhimu kwa afya zao.  

   

" Niliamua kuachana na kazi yangu nzuri ya Uhandisi yenye mshahara mnono nikalazimika kurudi nyumbani kuleta teknolojia ya kubadili maji magumu, yawe ya chumvi ama yana harufu ili yafae kwa kunywa na matumizi mengine," alisema Ngaiyamu. 


Ngaiyamu alisema uwekezaji wake huo unafaida kubwa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kutokana na matumizi makubwa ya chupa za plastiki ambayo yamekuwa ni tishio kwa uharibifu wa mazingira. 


"Jambo ili niliona ni fursa ya moja kwa moja kwani watu wanaweza kuja na ndoo wapate maji ya kunywa safi na salama bila kutumia chupa ndogo ndogo ambazo zinakuwa zikizagaa sehemu mbalimbali,."  aliongeza Ngaiyamu.

 

 

      Alisema lengo la mradi huu ni kurahisisha upatikanaji wa maji safi na salama karibu na makazi ya wananchi, huku ukipunguza gharama wanazokabiliana nazo.


Baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam wamempongeza Mhandisi Ngaiyamu kwa  kuanzisha uwekezaji huo ambao ni mkombozi kwao. 


"Tulikuwa tukitembea umbali mrefu kutafuta maji lakini hivi sasa tunayapata  mahali tulipo na kwa bei nafuu ni jambo zuri sana , “ alisema Mwajuma Khalid.

 

Furaha Alinanine alisema mwekezaji huyo anapaswa kupewa maua yake kwa kuwa na jicho liliona mbali na kuja na ubunifu huo aliouona Dubai hatua ambayo itapunguza au kuondoa kabisa hatari ya magonjwa yanayotokea kutokana na matumizi ya maji yasiyo salama.

   

         Kwa upande wake Salome  Kamugisha maarufu kwa jina la Mama Maakuli amesema huduma ya maji safi na salama imekuja kuwa mkombozi kwa akina mama husani wale wakipato cha chini ambao licha ya kujishughulisha na ujasiriamali bado pesa hatoshi kwa mahitaji muhimu ikiwemo ya kupata maji ya kunywa kwa wakati. 

      
" Mwandishi mimi sijui nimshukuru namna ipi Mungu  ambaye amempa uwezo huyu Mwekezaji  kwa kuweka kiosk hapa jirani na mgahawa wangu.

Hapa maji ni ya chumvi, tumeteseka sana kupata maji ya kunywa. Tunanunua barafu lakini haifai kitu ikizingatiwa hapa Bunju joto ni kali mno, hakika  Mungu ametujibu maombi yetu," alisema Kamugisha.

 

Naye Ashura Kinyonge mkazi wa Mbezi Beach kwa Zena ambako nako kuna kiosk kingine amesema wamepata suluhisho la usumbufu wa kuagiza maji ya chupa dukani mara kwa mara.

 

“Hapa kwa kweli nimekomboka, Mume wangu Said Kinyonge akitoka kazini kwake anapitia kwenye  kioski anabeba dumu la lita 5 kwa Shilingi 1000, linatusaidia kwa kutwa nzima familia ya watu watatu,” .


“Kiukweli siyo kumsifia mtu amejua kutusaidia, nikinunua lita mbili kwa Sh.400 nikaenda nayo kwenye ujarisiamali wangu yananisogeza hadi narudi nyumbani,” alisema Ashura.

 

Ashura aliongeza kuwa mbali na kuboresha afya za wananchi, mradi huu pia umefungua fursa za kiuchumi kwa baadhi ya wakazi wanaohusika katika uendeshaji wa vituo hivyo, jambo linalosaidia kuongeza kipato chao na kuboresha maisha yao kwa ujumla.


           Akizungumza baada ya kutembelea na kuzindua baadhi ya vituo hivyo, Waziri wa Habari na Teknolojia, Angela Kailuki, alimpongeza mwekezaji huyo kwa mchango wake kwa jamii.


Alisema juhudi hizo zinaunga mkono jitihada za serikali za kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu kwa urahisi.


"Hawa ndio watu  ambao serikali inawahitaji. Serikali yako inakutumikia kabla ya wewe kulalamika jiulize umeifanyia nini jamii inayokuzunguka.

 

“Maana serikali haina uwezo wa kuajiri kila muhitimu kwa wakati ambapo anahitaji ajira” alisema Waziri Kairuki.

 

Waziri huyo alihitimisha kwa nukuu ya Rais wa zamani wa Marekaani Bill Clinton enzi za utawala wake aliyesema ‘Kabla ya kuilalamikia Marekani jiulize wewe umeifanyia nini nchi hiyo’.


       Aidha, alihimiza kupanuliwa kwa mradi huo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi, hasa katika maeneo ambayo bado yanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama.


   Pamoja na kuwasaidia wananchi uwekezaji huu unakabiliwa na changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara jambo linaloathiri uzalishaji kwa asilimia 40.


Changamoto nyingine wizi wa miundo mbinu na mwitiko mdogo kwa wananchi wanaohudumiwa.


Akizungumzia ubora wa maji hayo kwa  mujibu wa Valentino mradi wa vioski umehakikiwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na pia mashine zinapima maji wakati zikizalisha na kuonyesha ubora na usafi wa maji( quality) pia wanatumia maabara za serikali kama  chuo cha maji Rwegalulila ( Rwegalulila Water Institute) na kufanya vipimo  na kujiridhisha juu ya ubora unaotakiwa.


   Gharama za kuanzisha kiosk cha maji safi na salama chenye viwango stahiki ni kati ya Shilingi milioni 24 hadi 32, ndani ya fedha hizo unapata mashine, tanki, vibali, ujenzi na ufungaji. 


  Kwa ujumla, uwekezaji huu unaonekana kuwa mwanga wa matumaini kwa wakazi wa Dar es Salaam, ukionesha namna sekta binafsi inavyoweza kushirikiana na jamii kutatua changamoto za msingi na kuboresha maisha ya wananchi.


   Wapo wanufaika wa mradi wa viosk vya maji safi na salama ambao idadi yao ni zaidi ya 30.


Miongoni mwao ni Michael  Kapaya ambaye amepata ajira sasa ana zaidi ya mwaka mmoja iliyomwezesha kumiliki pikipiki mpya ambayo amemwajiri kijana mmoja anayemletea   fedha.

   
“ Ninayo mengi ya kuelezea juu ya kampuni hiyo kwa zaidi ya mwaka sasa. Nimenunua samani za ndani, pikipiki ambayo nayo inaniingizia pesa”.

Nina wasaidia wazazi wangu, tofauti na mishahara ya makampuni mengine niliyokuwa nikiyafanyia kazi. Niko katika hatua za mwisho ili niweze kununua kiwanja nianze kujenga nyumba,” alisema Kapaya.


    Mwekezaji wa Dontino Water Refilling Co.Ltd ni kijana msomi na mbunifu ambaye ni mzalendo wa kweli aliyeamua kurudi nyumbani kuwasaidia watanzania na kutoa chachu ya ubunifu na uthubutu katika kile mtu anachofikiri kinaweza kuleta maendeleo kama siyo kupunguza umaskini nchini Tanzania.


Hivyo kama Taifa tunapaswa kuunga mkono jitihada zake kijana huyu wa Kitanzania badala ya kumkwamisha kwa sababu mbalimbali. 


Makala hii imeandaliwa na Magreth Kabyemela anayepatikana kwa namba 0767697690 na Dotto Mwaibale anayepatikana kwa namba 0754362990.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad

Pages