KIWANDA CHA KUONGEZA THAMANI ZAO LA PARACHICHI MKOA WA NJOMBE KUANZA RASMI FEBRUARI 2025 - UMOJA BANKING BLOG

Breaking

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, 10 January 2025

KIWANDA CHA KUONGEZA THAMANI ZAO LA PARACHICHI MKOA WA NJOMBE KUANZA RASMI FEBRUARI 2025


Mabadiliko makubwa ya kiuchumi Mkoa wa Njombe kupitia zao la parachichi yameanza kuonekana.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, akizungumza na Mkurugenzi wa Kampuni ya Avo Africa,Najib Karmal,  ambayo inajenga kiwanda cha kuongeza thamani zao la parachini wakati wa ziara yake ya kutembelea kiwanda hicho aliyoifanya Januari 10, 2025.

..........................................

Na Chrispin Kalinga, Njombe 


MKOA wa Njombe umeanza mwaka mpya wa 2025 kwa mafanikio makubwa katika sekta ya uwekezaji, kufuatia ziara ya Mkuu wa Mkoa, Anthony Mtaka, katika kiwanda kipya cha kuchakata mafuta ya parachichi kinachomilikiwa na Kampuni ya Avo Africa. 


Ziara hiyo imeonyesha juhudi za serikali za kuleta maendeleo kupitia uwekezaji wa kimkakati.


Kiwanda cha Avo Africa, ambacho kinatarajiwa kuanza uzalishaji rasmi mwezi Februari 2025, ni mradi wa kipekee unaolenga kushughulikia changamoto za wakulima wa parachichi. Zaidi ya hayo, mradi huu unalenga kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na kuchochea maendeleo ya kiuchumi. 


"Mwaka 2025 ni mwaka wa suluhisho wa vilio vya wakulima wa parachichi, kupitia kiwanda hiki, tunaenda kushuhudia mabadiliko makubwa ya kuongeza thamani ya mazao na kuchochea maendeleo ya kiuchumi." alisema Mtaka wakati wa ziara hiyo.


MAENDELEO YA KIUCHUMI NA FURSA ZA AJIRA 


Kiwanda hiki kinatarajiwa kutoa ajira zaidi ya 400, nyingi zikilenga vijana wa Njombe na maeneo jirani. Hii ni sehemu ya utekelezaji wa dira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha uwekezaji na kukuza ajira kwa vijana. Rais Samia mara nyingi amekuwa akisisitiza umuhimu wa wawekezaji kama nguzo ya maendeleo na ajira. 


"Kiwanda hiki siyo tu kwamba kitatoa ajira kwa mamia ya vijana, lakini pia kitapanua wigo wa maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla. Ni wakati wa wananchi wa Njombe kufaidika moja kwa moja na fursa hizi." alisema Mtaka.


Mtaka alisema Teknolojia ya kisasa inayotumiwa na kiwanda cha Avo Africa inahakikisha bidhaa zitakazozalishwa zitakidhi viwango vya kimataifa, na hivyo kuvutia masoko ya ndani na nje ya nchi. Hali hii inazidi kuimarisha nafasi ya Njombe kama kitovu cha uzalishaji wa parachichi barani Afrika.


NJOMBE: KITOVU CHA MAENDELEO ENDELEVU 


Akielezea juu ya uwekezaji huo Mtaka alisema ni mfano wa jinsi Mkoa wa Njombe unavyoweza kuwa sehemu muhimu ya mabadiliko ya kiuchumi kupitia ushirikiano wa kimataifa na uwekezaji wa ndani. Kiwanda hiki kinatoa matumaini mapya kwa wakulima wa parachichi na kuongeza thamani ya mazao yao.


" Kwa kila hatua, Njombe inazidi kujidhihirisha kuwa mshirika thabiti wa juhudi za serikali za kufanikisha Tanzania ya viwanda, na kuwa mfano wa mafanikio ya uwekezaji unaolenga maendeleo endelevu na ustawi wa jamii," alisema Mtaka.

MANUFAA MAKUBWA KWA WAKULIMA NA WANANCHI 


 Kwa upande wake  Mkurugenzi wa Avo Africa, Najib Karmal, alisema ujenzi wa kiwanda hicho  utakamilika mapema, na kinatarajiwa kuanza uzalishaji mwezi wa pili mwaka huu na kuwa kitakuwa na uwezo wa kununua zaidi ya tani 10,000 za parachichi kila mwaka kutoka kwa wakulima wa ndani kwa ajili ya uzalishaji.


Karmal ameipongeza Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji nchini , hali inayotoa fursa kwa kiwanda cha uzalishaji wa mafuta mjini Makambako kuwa sehemu muhimu ya kupunguza ombwe la upatikanaji wa mafuta.


"Mazingira ya uwekezaji yaliyoboreshwa na serikali yamekuwa msingi wa mafanikio ya miradi kama huu. Tunaamini kiwanda hiki kitakuwa chachu ya maendeleo kwa mkoa wetu na Tanzania kwa ujumla," alisema Kurmal. 

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, akisisitiza jambo wakati wa ziara hiyo kiwandani hapo.

Muonekano wa kiwanda hicho.

Mkurugenzi wa Avo Africa, Najib Karmal,  akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Athony Mtaka wakati wa ziara hiyo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad

Pages