GAVANA WA BENKI KUU AIPONGEZA BENKI YA DCB KWA KUKUZA MTAJI - UMOJA BANKING BLOG

Breaking

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, 10 January 2025

GAVANA WA BENKI KUU AIPONGEZA BENKI YA DCB KWA KUKUZA MTAJI

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba akizungumza wakati wa hafla ya kuorodheshwa Hisa Stahiki za Benki ya Biashara ya DCB kwenye soko Hisa la Dar es Salaam (DSE)

.......................................................

Na Mwandishi Wetu, Dar es  Salaam
 

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba ameipongeza Benki ya Biashara ya DCB kwa kuongeza mtaji wake kutoka shs bilioni 15 hadi shs bilioni 25.74 kupitia zoezi ya uuzaji wa Hisa Stahiki.

 

Pongezi hizo alizitoa jijini Dar es Salaam jana 10 Januari 2025, katika hafla ya kuorodheshwa hisa stahiki za benki ya DCB katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE). Gavana alisema mafanikio ya zoezi hilo sio tu kwa manufaa ya Benki ya DCB pekee bali pia ni kwa sekta nzima ya fedha ikionesha maono, uvumilivu, na nia thabiti ya uongozi wa benki, masoko ya mitaji, wanahisa, na wadau wake, ambao wameendelea kuamini katika uwezo wa benki hii na mchango wake katika mageuzi ya uchumi wa taifa.

 

“Umuhimu wa masoko ya mitaji katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi hauwezi kupuuzwa, kwa kutoa jukwaa la kukusanya mtaji wa muda mrefu, masoko haya huwezesha biashara kupanuka, kuleta ubunifu, na kuchangia katika uundaji wa ajira, mafanikio ya DCB yanadhihirisha nguvu ya masoko haya katika kukuza na kuimarisha uchumi wa nchi yetu.

 

“Ili benki iweze kuendelea inahitaji mambo makuu matatu, uongozi bora, bidhaa nzuri zinazoweza kuuzika sokoni na mtaji. Sisi kama Benki Kuu tuna Imani kubwa na uongozi wa benki yaani Bodi na Menejimenti ya DCB, bidhaa zake ni nzuri na sasa kwa ninafurahi kuona kwamba kupitia zoezi hili la mauzo ya Hisa Stahiki, DCB imefanikiwa kuongeza mtaji wake kutoka TZS bilioni 15 hadi kufikia TZS bilioni 25.7”, alisema Gavana Tutuba.

 

Pamoja na hayo Gavana alitoa pongezi kwa hatua ambazo DCB benki kwa kuipa vipaumbele vya maendeleo ya kitaifa, ikiwa ni pamoja na kuunga mkono wanawake wajasiriamali, wafanyabiashara wa masokoni, na makundi maalum kupitia bidhaa bunifu za mikopo kama huduma ya mkopo wa wanawake “Tausi,” mikopo ya Bodaboda na Bajaji, na Mikopo ya Sokoni.

 

“Kwa namna ya kipekee niipongeze Bodi, Menejimenti na Wanahisa wa DCB kwa hatua za kimaendeleo tokea kuanzishwa kwa benki, kwanza benki hii ilipata kibali cha Benki ya Kijamii (Microfinance) mwaka 2002, baada ya kufanya kazi vizuri, kuongeza mtaji na kukidhi vigezo vya benki kuu mwaka 2012 hadhi ya leseni ya benki ilipandishwa na kuwa Benki kamili ya kibiashara (Commercial Bank) na sasa kwa kuongeza mtaji, leo hii benki hii imetoka katika kundi la mabenki madogo na kuwa benki ya kundi la kati. Ninaamini mafanikio yaliyopatikana kupitia ongezeko hili la mtaji yataendela kuifanya DCB kuwa na matokeo mazuri na kuwa moja ya benki kubwa huo mbeleni”. Alisema Gavana.

 

“Benki Kuu ya Tanzania imejitolea kuunda mazingira wezeshi kwa taasisi za kifedha kustawi huku ikihakikisha uthabiti na uadilifu wa mfumo wa fedha ili kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi dhabiti wa Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan, mafanikio ya leo ya DCB ni ushahidi wa kile kinachoweza kufikiwa wakati vyombo vya udhibiti, taasisi za kifedha, na wadau wanaposhirikiana kufanikisha malengo ya Pamoja kuiunga mkono benki ili iweze kufanikiwa zaidi”, aliongeza gavana huyo.

 

Awali akizungumza mahali hapo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya DCB, Bi. Zawadia Nanyaro alisema suala la kuongeza mtaji wa benki yao linatokana na sheria na kanuni za Benki Kuu zinazotaka mabenki ya kibiashara kuwa na mtaji wa angalau shs bilioni 15 na nia ya kufanikisha mpango mkakati wa miaka mitano (2024-2028) ambao ulitoa kipaumbele kwenye suala zima la mtaji ikiwa na lengo la kukuza mtaji kutoka bilioni Tsh 15 (2024) hadi kufikia shilingi bilioni 61 ifikapo mwaka 2028. “Benki ya DCB tutaendelea kufanya biashara kwa kuzingatia vigezo, kanuni na miongozo yote inayotolewa na mamlaka za serikali ili kuendeleza uchumi wa nchi yetu kwa masilahi mapana ya wanahisa wetu, wadau, wateja na watanzania kwa ujumla”, alisema Bi. Zawadia.

 

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bw. Sabasaba Moshingi alisema, ongezeko la mtaji linatarajia kuleta matokeo mazuri zaidi yatayoleta tija kwa wanahisa wake, wadau na watanzania kwa ujumla, mtaji ukitumika kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo wadogo, kutoa mikopo kwa makundi maalumu kama wanawake, bodaboda, masokoni, walimu na wafanyakazi, kuboresha pia huduma za kibenki kwa njia ya kidigitali ili ziendane na wakati hivyo kukidhi mahitaji ya watanzania wenye kiu ya kupata huduma bora, za kifedha kwa urahisi na kwa gharama nafuu.

 

“Historia yetu inaonesha kwamba, mtaji wa kwanza wa benki ulikuwa Tshs bilioni 1.7 ulipatikana kutoka Halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam baada ya kuhimizwa na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2001 hayati Mhe. Benjamin Mkapa, ambapo benki yetu ilipata kibali cha kuendesha benki ya jamii (community bank) kutoka Benki Kuu mwaka 2002, ikifahamika kama benki ya wananchi wa Dar es Salaam. Mtaji wa benki uliendelea kuongezeka kupitia wanahisa waanzilishi na baadae wanahisa wengine waliwekeza katika benki kupitia masoko ya mitaji na hatimaye kuorodheshwa katika soko la hisa ikiwa ni benki ya kwanza kuorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), mnamo mwaka 2008.

 

“Natoa shukurani kubwa kwa wanahisa wetu walioshiriki katika mauzo ya Hisa Stahiki, niwaombe sana muendelee kuisaidia benki yetu katika kufanya biashara na benki, tunaamini tukifanya hivyo benki itapata faida kubwa, mtaji wa benki utaongezeka, pato la wanahisa litaongezeka, hivyo kuendelea kusukuma mbele ajenda ya Rais wetu shupavu, Mhe. Mama Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea wananchi maendeleo kupitia huduma za kifedha huku tukihakikisha huduma hizi zinawafikia watu wengi na kwa urahisi.

 

“Pia nitoe shukurani za pekee kwa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) kwa miongozo ambayo imewezesha kupata mafanikio katika mauzo ya Hisa Stahiki na kuwezesha kuorodhesha hisa hizi leo katika Soko la Hisa, aidha, napenda kutoa shukrani za dhati kwa kampuni ya iTrust Finance Limited ambao ni washauri kiongozi katika zoezi zima la uuzaji wa hisa wakiwa na timu ya wanasheria kutoka Endoxa na wahasibu kutoka Auditax, na kwa wanahisa wetu wote wakiwemo wamahisa wakuu Jiji na Halmashauri zote za mkoa wa Dar es Salaam, UTT - Amis, NHIF na wengineo”, alisema Bw. Moshingi.

 

Akizungumza katika hafla hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa DSE, Bw. Peter Nalitolela alitoa rai kwa watanzania kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana katika masoko ya mitaji huku Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bwana Nicodemus Mkama akisema mazingira wezeshi na shirikishi yaliyowekwa na Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ndio yaliyosababisha asilimia 100 ya waliojitokeza kununua hisa za DCB kwa watanzania binafsi na taasisi za kitanzania. 


“Niwapongeze DCB kwa kuwa benki ya kwanza nchini Tanzania kuorodheshwa katika soko la hisa la Dar es Salaam na kuendelea kuongeza mitaji kupitia masoko ya mitaji na dhamana. Pia niwapongeze wanahisa na Bodi ya DCB kwa kuwa benki na taasisi pekee katika makampuni yaliyoorodheshwa katika soko la hisa la Dar es Salaam kuwa na mwenyekiti mwanamke na anayeiongoza benki kwa mafanikio, hii inaendana sambamba na miongozo inayotolewa na Benki Kuu ya kuhakikisha benki zetu zinawapa wanawake kipaumbele katika nafasi za uongozi katika ngazi za juu”, aliongeza Bwana Mkama.

 

Viongozi wote waliwasihi wanahisa wa benki ya DCB kuendelea kushirikiana na benki ya DCB ili kuisaidia benki kukua, kupata faida na kuongeza dhamani ya wanahisa wake.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba ( wa tatu kushoto) akigonga kengele kuashiria  kuorodheshwa kwa Hisa Stahiki za Benki ya Biashara ya DCB kwenye soko Hisa la Dar es Salaam (DSE) jijini Dar es Salaam . 

Zoezi la uuzwaji wa Hisa Stahiki 97,646,913 zenye thamani ya shilingi 10,741,160,430 lilizinduliwa Novemba 11, 2024 na kukamilika Disemba 6 mwaka huo kwa mafanikio ya asilimia 100. Wengine Kutoka kushoto ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Itrust Finance, Bw. Faiz Arab, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Nicodemus Mkama, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa DCB, Bi. Zawadia Nanyaro, Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bw. Sabasaba Moshingi na Ofisa Mtendaji Mkuu wa DSE , Bw. Peter Nalitolela.Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya DCB, Bw. Sabasaba Moshingi akizungumza katika hafla hiyo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Biashara ya DCB, Bi. Zawadia Nanyaro akizungumza katika hafla hiyo. 

Picha ya pamoja
Picha ya pamoja

 Picha ya pamja

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad

Pages