....................................
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imezindua rasmi Kiwango cha kwanza cha sehemu
yake ya pili ya Hati Fungani ya NBC Twiga, yenye thamani ya shilingi bilioni
27.2, ikiwa ni hatua muhimu ya kuimarisha sekta ya biashara ndogo na za kati
nchini.
Hatua hii ya kimkakati ya benki hiyo inatajwa kuwa inalenga kuthibitisha
jitihada za benki hiyo katika kurahisisha upatikanaji wa mitaji miongoni mwa
wafanyabiashara hususani wajasiriamali ili kukuza maendeleo ya kiuchumi nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na benki hiyo mwishoni mwa wiki, hati fungani
hiyo ya miaka mitano tayari imeorodheshwa kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam
(DSE).
“Fedha zitakazopatikana kupitia Hati Fungani hii ya NBC Twiga zitatumika
kuwezesha mikopo rafiki kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati ambao kimsingi
tunawatambua kama uti wa mgongo wa uchumi wetu kama taifa,’’ alisisitiza Bw
Theobald Sabi, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, katika taarifa hiyo.
Bw Sabi alisisitiza kuwa kwa kuboresha upatikanaji wa mitaji hiyo muhimu kwa
wajasiriamali, benki ya NBC inadhamiria kufungua uwezo mkubwa wa ukuaji kwa
biashara hizo, hivyo kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa ujumla nchini.
“Malipo ya riba kwa wawekezaji yatafanywa kila nusu mwaka wakati wote wa hati
fungani hii itakayohitimishwa mwezi Oktoba, 2029. Jambo la msingi pia ni
kufahamu kwamba mapato yatokanayo na hati fungani hii hayatozwi kodi ya zuio
(withholding tax), na hivyo kuongeza mvuto wake kwa wawekezaji wa ndani na kimataifa,”
aliongeza.
Akizungumza kuhusu faida zinazoambatana na hati fungani hiyo, Bw Sabi alionesha
kuridhishwa na mchango wake katika kuimarisha sekta ya ujasiriamali nchini.
“Hati Fungani hii ya miaka mitano itaimarisha si tu sekta ya ujasirimali —ambayo
inawaajiri watu wengi katika nchi—bali pia itapanua upatikanaji wa mitaji na
kufungua fursa mpya za ukuaji wao,” alisisitiza.
Maoni ya Bw Sabi yanaakisi dhamira ya NBC ya kuendeleza maendeleo ya uchumi
endelevu kupitia ujumuishaji wa kifedha na msaada wa biashara zinazochipukia.
Uzinduzi wa Hati Fungani hiyo unakuja kama muitikio chanya kutoka kwa Mfuko wa
Dhamana za Sarafu za Ndani za Kiafrika (ALCB Fund) ambao ni mpango wa Umajumui
wa Afrika (Pan-Africanism) unaolenga kuwekeza katika hati fungani za kampuni na
mashirika kupitia sarafu za ndani.
Hivi karibuni, Mfuko wa ALCB ulifanya uwekezaji mkubwa wa fedha kiasi cha sh
bilioni 27.2 (takribani Dola za kimarekani milioni 10) katika hati fungani hiyo
ya NBC Twiga, hatua iliyoonesha imani ya mfuko huo katika kuuunga mkono
mikakati ya kifedha ya NBC.
Katika hatua inayoongeza imani na matarajio zaidi ya mpango huo, uwekezaji huo
wa Mfuko wa ALCB umewezeshwa kupitia ruzuku kutoka kwa Mfuko wa Kubadilisha
Sarafu (TCX) iliyotolewa kupitia Kituo chake cha Bei za Uundaji wa Soko la
Umoja wa Ulaya. Kituo hiki kinakusudia kuhamasisha matumizi ya sarafu za ndani
katika fedha za maendeleo, jambo ambalo ni muhimu katika kukuza utulivu wa
kiuchumi na ukuaji nchini.
“Hati Fungani ya NBC Twiga inatarajiwa kuchochea ukuaji wa mabadiliko,
ikinufaisha wajasiriamali na uchumi kwa ujumla, na hivyo kufungua milango kwa
siku nzuri zijazo katika mzunguko wa kifedha nchini.’’
“Tunapoendelea na mpango huu, tunabaki imara katika dhamira yetu ya kuimarisha
mifumo ya uchumi wa Tanzania, kuhakikisha kwamba wajasiriamali wanapata msaada
stahiki ili kuweza kustawi na kuchangia katika ajenda ya maendeleo ya kitaifa,”
alihitimisha.
No comments:
Post a Comment