Mfano wa Hundi ya Sh. Milioni 50 ikipokelwa.
.....................................
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
BENKI ya NMB, imetangaza udhamini wa Sh. Milioni 50 wa michuano ya Kombe la Mapinduzi ya Zanzibar (Mapinduzi Cup 2025), inayotarajia kuanza Januari 03, 2025 kwenye Uwanja wa Gombani visiwani Pemba, ambayo itashirikisha timu za Taifa, badala ya klabu za Tanzania Bara na Zanzibar kama ilivyozoeleka.
Sambamba na udhamini huo, NMB pia imekabidhi 'tracksuit' 100 zenye thamani ya Sh. Mil. 9 za kuvaa viongozi wa Serikali ya Zanzibar katika Siku ya Kitaifa ya Mazoezi (Januari 1, 2025), ambayo ni sehemu ya Shamrashamra za Miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, ambayo inafanyika chini ya kaulimbiu: 'Amani, Umoja na Mshikamano kwa Maendeleo Yetu - Mapinduzi Daima.'
Hafla ya makabidhiano ya hundi ya udhamini na 'tracksuit' hizo, imefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, ambako Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Zanzibar, Ahmed Jumaa Nassor, alimkabidhi Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bi. Fatma Hamad Rajabu, mbele ya Meneja Uhusiano wa NMB Zanzibar, Jaha Khamisi.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo baada ya kupokea hundi, Bi. Fatma aliishukuru NMB kwa mchango wao, ushirikiano na umoja wanaoonesha kwa Serikali ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi, na kuitaka kudumisha mashirikiano hayo kwa ustawi wa Zanzibar na maendeleo ya Wazanzibar kwa ujumla.
Alibainisha kuwa mchango na ushiriki wa NMB sio tu katika Sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar, bali iko mstari wa mbele daima kuchagiza maendeleo ya visiwa hivyo na wakazi wake na katika nyanja nyingi, ikiwemo michezo, ambako imejitoa vya kutosha kudhamini Kombe la Mapinduzi kwa miaka kadhaa na kuchangia ongezeko la ajira kupitia michezo.
"Wazanzibar wengi wanahudumiwa na NMB na uwingi wao unalenga kuiwezesha benki kukuza pato lao ili nao wanufaike na mchango wa maendeleo ya Zanzibar na watu wake. Tunawapongeza kwa kufadhili Siku ya Mazoezi Kitaifa, lakini pia kwa udhamini wenu mnono katika Kombe la Mapinduzi 2025.
"Tofauti na miaka yote ambako klabu hushiriki Kombe la Mapinduzi, mwaka huu zitacheza timu za Taifa, ikiwemo Zanzibar Heroes. Wito wetu kama Serikali, tunawataka Wazanzibar wajitokeze kwa wingi Uwanja wa Gombani Pemba, kuisapoti timu yao iweze kubakisha nyumbani taji la mashindano hayo," alisema Bi. Fatma.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Zanzibar, Ahmed Jumaa Nassor, alisema benki yake inajisikia fahari kuwa sehemu ya Shamrashamra za Mapinduzi ya Zanzibar kwa miaka 12 sasa na kwamba inatambua na inathamini mchango wa Serikali ya Zanzibar katika kuweka mazingira wezeshi ya wao kuhudumia Wazanzibar na kuunga mkono juhudi za maendeleo ya wananchi.
"NMB imekuwa mshirika mkubwa wa Serikali zote (Zanzibar na Tanzania), hivyo ni heshima kuendelea kuwa sehemu ya Shamrashamra za Miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
"Tuko hapa kufanya mambo mawili, yote yakihusiana na sherehe hizo zinazoanza Januari Mosi na kufikia ukomo wake Januari 13, siku moja baada ya kilele cha Miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
"Leo tunakukabidhi 'tracksuit' 100 za kuvaa washiriki wa Siku ya Mazoezi Kitaifa Zanzibar Januari Mosi, tukiamini kuwa mchango huu utatumika kama chachu katika muendelezo wa hamasa ya mazoezi miongoni mwa Wazanzibar, pia tunakabidhi kwako hundi ya udhamini wa mashindano ya Kombe la Mapinduzi, wenye thamani ya Sh. Milioni 50," alisema Ahmed na kuongeza:
"Udhamini huu pamoja na vifaa hivi, ni kilelezo na uthibitisho wa dhati kuwa NMB inathamini michezo, kwani afya zetu zinaimarika zaidi kupitia michezo na uimara wa afya ndio chachu ya kukua kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
"Ni fahari kubwa kwetu kuendelea kushirikiana na Serikali kwa miaka 12 ya NMB kuwa sehemu ya ukamilifu wa matukio hayo kwa kipindi chote hicho," alisisitiza Ahmed katika hafla hiyo iliyoshuhudiwa pia na maafisa wa wizara hiyo ya Habari, Vijana Utamaduni na Michezo pamoja na Wajumbe wa kamati ya kombe la mapinduzi 2025.
No comments:
Post a Comment