-Awapongeza Rais Samia na Museveni kwa msimamo wa uongezaji thamani madini
-Azitaka nchi za Afrika kuwa na mkakati wa pamoja wa uvunaji wa rasilimali Madini
-Uganda yavutiwa na maendeleo ya sekta ya madini nchini Tanzania
Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde akitoa hotuba wakati akishiriki Mkutano wa 13 wa Utajiri wa Madini Jijini Kampala, nchini Uganda Oktoba 2, 2024.
.................................
Kampala,Uganda
Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde amezitaka nchi za Afrika wazalishaji
wa madini mkakati kuweka usimamizi madhubuti wa rasilimali hizo ili zisaidie
kukuza uchumi wa Afrika kwa kuhakikisha unakuwepo mkakakati imara wa kuongeza
thamani madini hayo katika nchi wazalishaji.
Mh. Mavunde ameyasema hayo tarehe 02 Oktoba, 2024 alipokuwa akitoa hotuba yake wakati
akishiriki Mkutano wa 13 wa Utajiri wa Madini Jijini Kampala, nchini Uganda.
"Kipekee naomba nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Uganda, Mheshimiwa
Yoweri Kaguta Museveni kwa uamuzi wake thabiti wa hivi karibuni wa kukataza
usafirishaji wa madini ghafi nje ya nchi. Hii ni hatua muhimu sana kwa
maendeleo ya sekta ya madini na wananchi wa Jamhuri ya Uganda"
"Sisi Tanzania, tulishafanya uamuzi huo wa kukataza usafirishaji wa
madini ghafi nje chini ya uongizi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tumetamka bayana kwamba mwekezaji yeyote
atayehitaji kuwekeza kwenye uchimbaji wa madini mkakati ni sharti aoneshe
mpango kabambe wa uongezaji thamani nchini Tanzania", alisisitiza Mhe.
Mavunde.
Aidha, Waziri Mavunde alieleza kwamba, sekta ya madini imeendelea kukua na
kufanya vizuri ambapo kwa mwaka 2023, mchango wake kwenye pato la taifa ulifikia asilimia 9. Pia,
asilimia 56.2 ya thamani ya mauzo ya bidhaa zote nje ya Nchi yalitokana na
sekta ya madini, ambapo ilikadiriwa kuwa na thamani ya Dola za Kimarekani
Bilioni 3.5.
Vilevile, Mhe. Mavunde alieleza kwamba kwa upande wa maduhuli, asilimia 60
huchangiwa na wachimbaji wakubwa na asilimia 40 hutokana na wachimbaji wadogo.
Hali hiyo imeifanya Serikali ya Tanzania kuendelea kuweka mkazo katika
kuwasimamia na kuwaongoza wachimbaji wadogo ili wazalishe kwa tija na kuongeza
mchango wao kwenye uchumi wa Nchi.
Pia, Waziri Mavunde alieleza kwamba ili Nchi iweze kunufaika na madini
mkakati ni lazima iwekeze fedha nyingi kwenye utafiti ili kufahamu kiasi cha
madini hayo kilichopo na kuvutia wawekezaji. Alieleza kuwa katika hilo,
Tanzania tayari imekuja na Mpango wa Vision 2030 wenye lengo la kuongeza eneo
la utafiti wa kina kwa kurusha ndege kutoka asilimia 16 ya sasa na kufikia
asilimia 50 ifikapo Mwaka 2030.
Ni ukweli usiopingika kwamba Tanzania imepiga hatua katika kuendeleza sekta
ya madini ukilinganisha na Uganda, na kupelekea Mhe. Mavunde kueleza wazi kuwa
yupo tayari kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kushirikiana na kubadilishana uzoefu na Uganda ili waweze kunufaika na
rasilimali madini iliyopo nchini kwao.
Akihitimisha hotuba yake, Waziri Mavunde alisisitiza kwamba, Nchi za Afrika
ili ziweze kunufaika na fursa ya kuongezeka kwa mahitaji ya madini mkakati
duniani kama graphite, nikeli na cobalt ni lazima ziweke mikakati ya pamoja ya
kuhakikisha zinanufaika na uchimbaji na uongezaji wa thamani madini hayo ndani ya
nchi zao ili kulinda ajira, kuongeza mapato na ukuaji wa uchumi kwa ujumla.
Awali, katika mkutano huo akitoa hotuba ya sekta ya madini, Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Jamhuri ya Uganda, Mhe.Dkt. Ruth Ssentamu alibainisha kwamba Uganda imejipanga kuona sekta ya madini hususan madini mkakati yananufaisha Taifa, na kwamba wapo tayari si tu kujifunza kutoka Tanzania ambao wamepiga hatua kubwa kwenye sekta ya madini bali pia kushawishi uwekezaji wa fedha nyingi kwenye utafiti ili kuongeza ufanisi wa sekta ya madini ambayo kwa zaidi ya asilimia 80 imejumuisha wachimbaji wadogo.Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde akisisitiza jambo kwenye mkutano huo.
Majadiliano yakifanyika kwenye mkutano huo.Mawasilisho yakifanyika.
Taswira ya mkutano huo.
Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde akiwa katika picha ya pamoja na wadau kwenye mkutano huo
Picha ya pamoja mbele ya bango la mkutano huo
Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde akiwa na washiriki wenzake katika mkutano huo.
No comments:
Post a Comment