Leo, tarehe 1 Oktoba 2024, Kampuni ya ITO
EN LTD, kampuni tanzu ya Tully’s Co. Ltd., inayomiliki migahawa maarufu ya
Tully’s Coffee, imezindua aina mbili mpya za kahawa ya Tanzania, nchini Japan.
Aina hizo za kahawa ya Tanzania ni BARISTA’S ROAST KILIMANJARO na KIBO
TARIME SWEET WASHED, kutoka mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.
Uzinduzi huo umeongeza uhakika wa
upatikanaji wa kahawa ya Tanzania kupitia migahawa maarufu nchini Japan ya
TULLY’S ambapo, mwezi Machi mwaka huu, ITOEN kwa kushirikiana na TULLY’S
walizindua kahawa aina tatu za Tanzania, TULLY’s COFFEE BARISTA BLACK
KILIMANJARO; TULLY’S COFFEE MY HOME BLACK KILIMANJARO; na TULLY’S COFFEE
BARISTA ROAST COLD BREW – KILIMANJARO BLEND, zilizotoka maeneo ya Tarime,
mkoani Arusha na mashamba ya GDM yaliyoko Mbozi mkoani Mbeya.
Aidha, uzinduzi huo kumeifanya TULLYS
kuongoza kwa uuzaji kwa wingi wa kahawa ya Tanzania unaojumuisha, aina saba za
kahawa hiyo, ndani ya miaka miwili zikiwemo, kahawa za GDM FULL WASHED na GDM
NATURAL za Mashamba ya GDM mkoani Mbeya, zilizozinduliwa mwezi Agosti, mwaka
jana.
Hafla ya Uzinduzi huo ilifanyika katika
moja ya Migahawa ya TULLY’S uliopo kwenye Stesheni Kuu ya Tokyo ya Reli ya
Mwendokasi nchini Japan (JR LINE – TOKYO STATION) ambayo, iliongozwa na Rais wa
ITO EN LTD, Bw. Daisuke Honjo pamoja na Rais wa Migahawa ya TULLY’S, Bw. Yoshio
Kobayashi; na kuhudhuriwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Japan.
Uzinduzi huo pia ulipambwa na zoezi la
uonjaji wa kahawa ya Tanzania lililoshirikisha wataalam wa kahawa (baristas)
wapatao 10 wa maeneo mbalimbali nchini Japan; na makampuni mengine makubwa
ya kahawa ya Japan ya MARUBENI, MITSUI na ECOM, yenye ubia na Tanzania.
Kampuni ya ITO EN Ltd., ni kampuni
inayoongoza kwa biashara ya vinywaji nchini Japan ambayo, ni kampuni tanzu ya Tully’s
Coffee inayomiliki migahawa ya kahawa takriban 700 nchini Japan na imejipatia umaarufu mkubwa katika biashara ya uuzaji
wa kahawa za aina mbalimbali duniani.
Kuzinduliwa kwa aina nyingine mbili mpya za kahawa nchini
Japan, kunaendelea kupandisha zaidi uhakika wa soko la kahawa ya Tanzania,
Japan ambayo imejizolea umaarufu mkubwa kwa ubora na radha ya aina yake na
kupelekea kupewa jina maarufu la kibiashara la Kilimanjaro Coffee.
Kilimanjrao Coffee ni miongoni mwa brand tatu duniani zinazopendwa
zaidi Japan; na jina hilo hutumika nchini humo kwa kahawa zinazozalishwa
Tanzania pekee, kwa kutambua kivutio kikubwa cha Mlima Kilimanjaro uliopo
nchini Tanzania.
Kwa sasa, Tanzania inauza kahawa yake Japan kwa wastani
wa asilimia 34 ya kahawa inayolimwa nchini kutoka asilimia 32 ya mwaka jana,
ambayo ni sawa na wastani wa kilogramu million 15 (tani 15,000) ya kahawa yote
ya Tanzania inayouzwa nchini Japan. Takwimu hizo zinaendelea kuiweka Japan kuwa
mnunuzi mkubwa na namba moja (1) wa kahawa inayolimwa nchini.
IMETOLEWA NA UBALOZI WA TANZANIA NCHINI JAPAN
TOKYO
TAREHE 01 OKTOBA 2024
Kahawa hiyo ikiwa tayari ipo sokoni
Kahawa hiyo ikiandaliwa wakati wa uzinduzi.
Wadau mbalimbali wakiwa wamejipanga foleni tayari kwa kuionja kahawa hiyo.
Kahawa hiyo ikioneshwa kwa wadau wakati wa hafla hiyo ya uzinduzi.
No comments:
Post a Comment