……..................................
Na Noel Rukanuga, Dar es Salaam
Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu ya
Tanzania (BoT) imesema hali ya uchumi imeendelea kuimarika kwa
kumechangiwa kwa kiasi kikubwa ukuaji imara wa mikopo kwa sekta binafsi na
utulivu wa sekta ya fedha katika robo ya pili ya 2024.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julia 4, 2024 Jijini Dar es Salaam
wakati akitoa taarifa ya Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ya Bodi ya Wakurugenzi
wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Naibu Gavana wa BoT, Dkt. Yamungu Kayandabila,
amesema Kuwa tathmini mwenendo wa uchumi wa dunia, kamati ilibaini kuimarika
kwa shughuli za kiuchumi katika nchi nyingi kwa robo ya kwanza na ya pili ya
mwaka 2024″ amesema Dkt. Kayandabila.
Pia Dkt. Kayandabila amesema kuwa kamati imeamua riba ya benki Kuu (CBR)
kuendelea kuwa asilimia 6 kwa robo mwaka itakayoishia Septemba 2024 ili kuleta
tija katika masuala mbalimbali ya maendeleo.
“Maamuzi hayo yamezingatia mtazamo chanya wa uchumi wa dunia, ambapo
matarajio ni kuendelea kupungua kwa mfumuko wa bei katika nchi nyingi,
kuimarika kwa ukwasi katika masoko ya fedha duniani pamoja na kushuka kwa bei
za bidhaa katika soko la dunia” Dkt. Kayandabila.
Amesema kuwa kamati inatarajia uchumi wa ndani kuendelea kukua kwa kasi,
sanjari na upatikanaji wa chakula cha kutosha, na kupungua kwa kasi ya kushuka
kwa thamani ya shilingi kufuatia ongezeko la mapato ya fedha za kigeni kutokana
na shughuli za utalii pamoja na mauzo ya dhahabu na mazao ya biashara na
chakula.
Amesema kuwa mfumuko wa bei umeendelea kupungua, sanjari na kuimarika kwa
ukwasi katika masoko ya fedha duniani, na benki kuu katika nchi nyingi kuanza
kupunguza viwango vya riba.
Amefafanua kuwa bei ya mafuta ghafi ilipungua, licha ya kuongezeka kidogo
mwishoni mwa mwezi Juni 2024, huku akieleza kuwa bei ya dhahabu iliendelea kuwa juu,
ikiashiria dhahabu kuendelea kutumika kama uwekezaji mbadala katika mazingira
ya kushuka kwa thamani ya sarafu mbalimbali na migogoro ya kisiasa duniani.
Kuhusu mwenendo wa uchumi wa Tanzania, Kamati imeridhishwa na kuendelea
kuimarika kwa shughuli za kiuchumi, kutokana na utekelezaji wa sera thabiti na
maboresho mbalimbali yenye lengo la kukuza uchumi.
Amefafanua kuwa mikopo ya sekta binafsi nakadiriwa kukua kwa wastani wa
asilimia16.4 ikilinganishwa na asilimia17.1 katika robo iliyotangulia.
“Sekta ya benki imendelea kuwa na ukwasi na mtaji wa kutosha huku
ikitengeneza faida na amana, rasilimali na mikopo imeendelea kuongezeka, ubora
wa rasilimali za benki umeendelea kuimarika, kufuatia kupungua kwa kiwango cha
mikopo chechefu hadi asilimia 4”
Dkt. Kayandabila amesema kuwa mikopo ya sekta binafsi inatarajiwa kuendelea
kuongezeka katika kipindi kijacho cha mwaka 2024 kutokana na kuimarika kwa hali
ya uchumi wa dunia na wa ndani.
Amesema kuwa utekelezaji wa bajeti ya Serikali umeendelea kuwa wa
kuridhisha huku ukichagiza utekelezaji wa sera ya fedha.
Mapato ya ndani kwa Tanzania Bara yanakadiriwa kufikia asilimia 95 ya
lengo, huku upande wa Zanzibar, mapato yanakadiriwa kuvuka lengo kwa asilimia
0.3 kutoka na maboresho katika usimamizi wa kodi na kuongezeka kwa utayari wa
wananchi kulipa kodi katika mwaka 2024/25.
Dkt. Kayandabila amesema kuwa akiba ya fedha za kigeni iliendelea kuwa ya
kutosha kwa kuwa na zaidi ya dola za marekani bilioni 5, kiasi kinachotosheleza
uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa zaidi yamiezi 4.
Amesema kuwa upatikanaji wa fedha za kigeni uliimarika kiasi, mwishoni mwa mwezi Juni 2024, kutokana na ongezeko la fedha za kigeni kutoka kwenye mauzo ya tumbaku, dhahabu na shughuli za utalii.
No comments:
Post a Comment