NAIBU Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi ametembelea makao makuu ya kampuni ya Vodacom Tanzania kwa lengo la kujifunza namna kampuni hiyo inavyoendesha shughuli zake pamoja na kutatua changamoto wanazokutana nazo wateja wao.
Akizungumza wakati wa kikao chake na uongozi wa Vodacom kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam, Mhandisi Mahundi amesema kiu ya Serikali ni kuona wananchi wanaendelea kupata suluhu ya changamoto wanazokutana nazo katika huduma za mawasiliano.
Sambamba na kuipongeza kampuni hiyo kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuwaunganisha watanzania na huduma za mawasiliano, Mhandisi Mahundi ametoa rai kwa kampuni hiyo kuongeza wigo wa utoaji wa elimu kwa umma ili wateja wajue namna ya kutatua changamoto wanazokutana nazo za kiteknolojia na zile za kawaida.
Awali Mkurugenzi wa Kitengo cha Mtandao cha kampuni ya Vodacom Tanzania, Bw. Andrew Lupembe akiwasilisha taarifa ya mtandao wa kampuni hiyo amegusia namna kampuni hiyo inavyoshirikiana na Serikali katika kuongeza wigo na kuboresha huduma za mawasiliano nchini.
Bw. Lupembe amezungumzia ushirikiano wa Vodacom na Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umefanikisha ujenzi wa minara 306 inayotoa huduma za mawasiliano katika vijiji 1,184, na mkataba wa ujenzi wa minara 190 uliosainiwa mwaka jana kati ya Serikali na Vodacom utekelezaji wake unaendelea.
Naye Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kampuni hiyo, Bi. Zuweina Farah amesema utekelezaji wa Sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi umesaidia sana kupunguza changamoto nyingi za wateja kwasababu washirika wengi wa Vodacom wameanza kuitekeleza hivyo kuomba Serikali iendelee kutoa elimu zaidi kuhusu sheria hiyo katika makundi yote ya kijamii.
No comments:
Post a Comment