.........................................
NA: JOSEPHINE MAJULA, WF, TABORA
Taasisi za Uwekezaji nchini zimetakiwa kuongeza wigo wa kujitangaza na
kuwaelimisha wananchi kuhusu huduma wanazotoa ili kuongeza Wawekezaji na
kuiongezea Serikali mapato.
Ushauri huo umetolewa na Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora,
baada ya kumalizika kwa semina ya elimu ya fedha iliyotolewa na Wizara ya Fedha
iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mkoa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kupata elimu hiyo, Afisa Kilimo
wa Mkoa wa Tabora Bi. Eunice John, alisema kuwa Watumishi ni wengi ila hawana
elimu ya uwekezaji, bidhaa zinazopatikana katika Taasisi za Uwekezaji na
vihatarishi vilivyopo ili wafanye maamuzi sahihi katika kuwekeza.
“Binafsi sijawahi kupata elimu kutoka taasisi ya Uwekezaji yoyote hapa
nchini zaidi ya kusikia kwa watu, kuna fursa nzuri katika taasisi hizo zenye
faida kubwa ukiwekeza mtaji mkubwa” alisema Bi. Eunice John.
Alisema kuwa kila mtumishi anahitaji sana elimu katika masuala ya uwekezaji
ili aweze kufanya maamuzi ya kuwekeza ili kujiongezea kipato na kukuza uchumi,
na kwamba bila kupata elimu ya huduma zinazotolewa na kujua upatikanaji wa
faida hakuna mwananchi ataweka fedha zake kwenye taasisi hizo.
Naye Mtumishi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw. Martin Peter,
alisema kupitia elimu ya fedha aliyoipata ataanza kujiwekea akiba na
atajiepusha ya matumizi yasiyo ya lazima ambayo hayamuongezei kipato.
“Nitaendelea kuwa Balozi kwa Watumishi wenzangu ili elimu niliyoipata
ikawanufaishe nao na kuwashawishi kujijengea utamaduni wa kujiwekea akiba na
kufanya uwekezaji ili watakapo staafu wasitetereke kiuchumi na kupata magonjwa
ambayo yanatokana na mawazo ya kukosa fedha ya kukidhi mahitaji”, alisema Bw.
Martin Peter.
Naye Afisa Uhusiano na Elimu kwa Umma Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na
Dhamana (CMSA), Bi. Stella John, aliwapongeza watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa wa Tabora kwa kujitokeza kwa wingi kupata elimu ya fedha.
“Mwitikio umekua mkubwa sana kwa Watumishi hawa, naamini elimu tuliyowapatia
wameielewa vizuri hali iliyosababisha watumishi wengi kuonesha nia ya kufungua
akaunti na kuahidi kufanya uwekezaji, lakini pia kuna watumishi wengine
tumewafungulia akaunti hapa hapa za mifuko mbalimbali kwa ajili ya kufanya
uwekezaji, alisema Bi. Stella John.
Wizara ya Fedha inaendelea na zoezi la utoaji elimu kwa wananchi wa makundi mbalimbali mkoani Tabora katika Wilaya nne ya Sikonge, Urambo, Uyui na Tabora Manispaa, ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na elimu ya huduma ndogo za fedha. Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bi. Limi Bulugu, akieleza umuhimu wa kuweka akiba kwa Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, wakati wa semina ya elimu ya fedha kwa Watumishi hao iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano mkoani hapo.
Baadhi ya Watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, wakifuatilia mada mbalimbali kuhusu elimu ya huduma ndogo za fedha zilizotolewa na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali mkoani Tabora.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WF, Tabora)
No comments:
Post a Comment