SERIKALI KUU YAPOKEA GAWIO LA BILIONI 27.4 KUTOKA BENKI YA CRDB - UMOJA BANKING BLOG

Breaking

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, 23 June 2024

SERIKALI KUU YAPOKEA GAWIO LA BILIONI 27.4 KUTOKA BENKI YA CRDB

 Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amesema kuwa Serikali imepokea gawio la kiasi cha shilingi bilioni 27.4 kutoka Benki ya CRDB kutokana na Serikali Kuu kumiliki asilimia 21 ya Benki hiyo kupitia Mfuko wa Uwekezaji wa Pamoja na Serikali ya Denmark (DIF)

Hayo yamesemwa jijini Dodoma kwa niaba yake na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, wakati wa hafla ya Benki ya CRDB kuikabidhi gawio la mwaka 2023.

Prof. Mkumbo alisema kuwa gawio hilo litatumika kuwaletea maendeleo wananchi hasa katika kuimarisha sekta ya afya kwenye eneo la miundombinu na kusaidia upatikanaji wa dawa na vifaatiba.

”Nimefurahi pia kuona taasisi na mashirika ya Serikali na Halmashauri pia wanapokea gawio la jumla ya shilingi bilioni 24.32, hivyo, jumla kuu ya gawio tunalolipokea leo ni shilingi bilioni 51.72”, alisema Prof. Mkumbo.

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeongeza vituo vya afya kutoka 8,549 mwaka 2021 hadi vituo 9,693 mwaka 2024, ikiwa ni pamoja na zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, rufaa, kanda na zile za Taifa.

Alisema ongezeko hilo pia limekwenda sambamba na kuongezwa kwa vifaatiba vya kisasa vya uchunguzi wa magonjwa ikiwemo MRI kutoka 7 hadi 13, CT-Scan kutoka 12 hadi 45, Digital X-RAY kutoka 147 hadi 346, Ultrasound kutoka 476 hadi 668, Echocardiogram kutoka 95 hadi 102, Cathlab kutoka 1 hadi 4, na kununua Pet Scan 1 inayotumika kutolea huduma kwenye matibabu ya saratani.

Prof. Mkumbo amewapongeza viongozi wa Benki ya CRDB kwa utendaji mahiri ulioiwezesha Benki kuendelea kupata faida na kutoa gawio kwa Serikali na wanahisa wengine, kuwa vinara katika kulipa kodi, na kuongeza huduma jumuishi za fedha ikiwa ni pamoja na kutoa huduma katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay, alisema kuwa kutokana na matokeo mazuri ya kifedha iliyopata Benki kwa mwaka 2023, wanahisa wa Benki hiyo katika Mkutano Mkuu walipitisha azimio la gawio la shilingi 50 kwa kila hisa ambalo ni ongezeko la asilimia 11 ikilinganishwa na gawio la shilingi 45 kwa mwaka 2022.

Alisema kuwa jambo hilo linaonesha ukuaji endelevu wa uwekezaji wa wanahisa ndani ya Benki hiyo ambapo jumla ya gawio lote lililotolewa mwaka huu ni shilingi bilioni 130.6 sawa na asilimia 31.8 ya faida halisi iliyopatikana.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mhe. Olan Manase Njenza (Mb), alisema kuwa kazi kubwa imefanywa na Serikali katika kuboresha sekta ya Benki na gawio hilo ni matunda ya uwekezaji wa muda mrefu wa Serikali.

Ameziomba Benki kuangalia namna bora ya kuwekeza ili kuboresha uchumi wa Tanzania katika sekta za Kilimo, madini, utalii na sekta nyingine za uzalishaji.






 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad

Pages