NA: JOSEPHINE MAJULA, WF, TABORA
Katibu Tawala Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya amewataka Viongozi, Watumishi
na Wananchi mkoani humo kuchangamkia fursa za uwekezaji katika Masoko ya Mitaji
kwenye Taasisi rasmi zilizopewa dhamana na Serikali kufanya shughuli za
uwekezaji kisheria ili kuweza kupata faida na kujikwamua kiuchumi.
Dkt.Mboya, alitoa rai hiyo alipokutana na Timu ya wataalamu ya Wizara ya
Fedha ambao wamefika mkoani humo kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi
mbalimbali wakiwemo Watumishi, Wafanyabiashara na Wajasiriamali.
“Wananchi mkoani Tabora tuamke, tutumie vizuri elimu ya fedha tuliyoipata
hususan katika eneo la Uwekezaji ili tuweze kufanya maamuzi sahihi katika
kuwekeza ikiwemo kupelekeza fedha sehemu sahihi ili uweze kupata faida”,
alisema Dkt. Mboya.
Aliipongeza Wizara ya Fedha kwa kuendelea kutoa elimu ya fedha katika mikoa
mbalimbali na kuwahamasisha wananchi kutumia taasisi rasmi za fedha
zinazotambuliwa na Serikali.
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii na Mratibu wa Huduma Ndogo za
Fedha Wilaya ya Uyui, Bw. Cledus Mbawala, alisema kuwa katika ngazi ya Wilaya,
Ofisi yake imekuwa ikifanya ufuatiliaji na kuhakikisha Taasisi zote
zinazojihusisha na masuala ya fedha zinakuwa na leseni kutoka Benki Kuu ya
Tanzania na zinafuata sheria na taratibu katika kutekeleza majukumu yake.
Naye Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara
ya Fedha, Bi. Limi Bulugu, alisema kuwa wamefika mkoani Tabora kutoa elimu ya
fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali katika Wilaya nne za Uyui, Urambo,
Sikonge na Tabora Manispaa.
“Tunawapongeza wananchi kwa kuendelea kujitokeza kwa wingi kupata elimu ya
fedha kwa kuwa itawasaidia kupanga matumizi ya fedha wanazopata, wataweza
kujiwekea akiba, watakuwa makini kuchukua mikopo kwenye Taasisi rasmi, za fedha
na watafanya uwekezaji na kujikwamua kiuchumi”, alisema Bi. Bulugu.
Wizara ya Fedha inaendelea na zoezi la utoaji elimu kwa wananchi kuhusu huduma ndogo za fedha katika mikoa ya Tabora, Simiyu na Shinyanga ikiwa ni mwendelezo wa kutoa elimu ili kuhakikisha kila mtanzania anafikiwa na elimu ya huduma ndogo za fedha.
Katibu Tawala Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya, akizungumza na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha ambayo ilifika ofisini kwake kujitambulisha na kuelezea njia watakazo tumia kufikisha elimu ya huduma ndogo za fedha katika Wilaya ya Urambo mkoani Tabora.
Baadhi ya Wananchi wa Wilaya ya Uyui, wakifuatilia mada mbalimbali zilizotolewa na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha ambayo ipo mkoani Tabora kutoa elimu ya fedha kwa Wananchi wa makundi mbalimbali wakiwemo Watumishi, Wafanyabiashara na Wajasiriamali.Mkazi wa Wilaya ya Uyui, Bw. Musa Salum, akiuliza swali kuhusu kiwango cha riba zinachotambulika na Serikali kwa Timu ya Watalaamu ya Wizara ya Fedha ambayo ipo wilayani humo kutoa elimu ya fedha kupitia mada mbalimbali ikiwemo kuweka akiba, uwekezaji na mikopo mkoani wa Tabora.
Baadhi ya Wananchi wa Wilaya ya Uyui, wakiwa wamevaa tisheti walizopewa kama zawadi baada ya kujibu maswali wakati wa semina iliyotolewa na Wizara ya Fedha ambayo ipo wilayani humo kutoa elimu ya fedha katika mada mbalimbali ikiwemo kuweka akiba, uwekezaji na mikopo mkoani wa Tabora.
No comments:
Post a Comment