Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko akikata utepe kuashiria kufungua maonyesho ya siku tatu ya Mifugo yaliyoandaliwa na Chama cha Wafugaji Kibiashara (TCCS) na kufadhiliwa na Benki ya NMB yaliyofanyika Bagamoyo Mkoa wa Pwani..
.................................
Na Mwandishi Wetu, Bagamoyo
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko ameipongeza Benki
ya NMB kwa kuanza kutoa bima ya mifugo inayolenga kupunguza hatari kwa wafugaji
kote nchini.
Bidhaa hii ya bima ni sehemu ya dhamira ya benki hiyo ya kuwalinda wafugaji
dhidi ya hasara za kifedha zinazoweza kutokea kwa wafugaji zikiwemo hatari za
ghafla au zisizotarajiwa.
Akizungumza kwenye banda la benki hiyo wakati wa kufunga maonyesho ya siku
tatu ya Mifugo yaliyoandaliwa na Chama cha Wafugaji Kibiashara (TCCS) na
kufadhiliwa na Benki ya NMB na kukutanisha na wadau mbalimbali wa sekta ya
mifugo mwishoni mwa wiki wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani , Biteko alisema kuwa bima ya mifugo ni dhana mpya
katika soko la Tanzania na kuitaka benki hiyo kuongeza wigo wake ili
kuwanufaisha wafugaji wengi nchini.
"Kwa kweli nimeifurahia hii dhana ya bima ya mifugo na nakiri kwamba
ni dhana mpya katika soko la Tanzania,” alisema.
Biteko alisema ingawa idadi ya ng’ombe imeendela kukua siku hadi siku na
kufikia milioni 37 katika miaka ya hivi karibuni, mchango wa sekta ya mifugo
katika uchumi wa nchi bado ni mdogo sana.
"Hii ni kwa sababu ya kutegemea ufugaji wa ng'ombe wa kizamani. Wizara
ya Mifugo na Uvuvi inatakiwa kuja na mikakati mipya ya kuwawezesha wafugaji
kubadili ufugaji na kuwawezesha kufuga kisasa,” alisema.
Biteko alisema tayari Serikali imekamilisha Mpango Kabambe wa Sekta ya
Kilimo unaolenga kutatua changamoto kadhaa zinazoendelea kukwamisha maendeleo
endelevu ya sekta ya kilimo nchini.
"Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kuleta mabadiliko katika sekta
ya kilimo," aliongeza.
Awali, Mkuu wa Idara ya Kilimo, Wateja Wakubwa ya Benki ya NMB, Christopher
Mwalugenge alisema bima ya mifugo inayotolewa na benki yake inajumuisha aina
kadhaa za hatari zinazohusiana na mifugo, zikiwemo vifo na wizi wa mifugo.
"Kama benki, tunaelewa kuwa mifugo ni vitega uchumi muhimu hivyo
ilikulinda wafugaji dhidi ya upotevu wa ghafla, tumekuja na hii bima mifugo
ambayo inaghariu kiasi cha shilingi elfu 20 tu kila mfugo kwa mwaka,"
Aliongeza kuwa benki yake imejikita katika kulinda vitega uchumi vya
wafugaji kwa kutoa bima ya mifugo iliyoboreshwa ili kupata mustakabali wa
mifugo yao pamoja na mustakabali wa biashara zao.
Kwa upande wake Naibu Waziri Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti wakati wa
hafla hiyo aliwataka wafugaji kuachana na ufugaji wa asili na kuanza ufugaji wa
kisasa ili kuleta tija katika biashara zao.
"Kama wizara, tumekuwa tukitoa elimu na kuhamasisha wafugaji kuachana na ufugaji wa kizamani na kuanza kufuga kisasa lakini mwitikio bado ni mdogo sana. Wafugaji wengi nchini Tanzania wanaendelea kutegemea ufugaji wa asili ambao unadhoofisha tija. Siku zimepita ambapo mfugaji anasafiri umbali mrefu kutafuta malisho,” alisema.
No comments:
Post a Comment