......................................
Na Saidina Msangi, WF, Dodoma.
Serikali imesema kuwa mwaka 2017 kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa
biashara, ilitoa mwongozo wa pamoja wenye dhima ya kuunganisha tozo na kodi
mbalimbali kwa nia ya kupunguza wingi wa tozo na kodi ili kuimarisha mazingira
ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini.
Hayo yameelezwa bungeni, jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad
Hassan Chande (Mb), wakati akijibu swali la Mbunge wa Mpendae, Mhe. Toufiq
Salim Turky, aliyeuliza Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kunakuwa na
muunganiko wa kodi ili kupunguza utitiri wa kodi usio wa lazima kwa wawekezaji.
Mhe. Chande alisema kuwa mpango huu umekuwa ukitekelezwa kwa ufanisi mkubwa
kupitia marekebisho mbalimbali ya Sheria ya Fedha, kuanzia mwaka 2018 hadi
2023, kwa kupunguza na kuondoa kodi na tozo mbalimbali.
‘‘Serikali itaendelea kuhakikisha makubaliano yaliyofikiwa na wadau
yanakamilishwa kama yalivyopangwa ili kuimarisha mazingira ya ufanyaji biashara
nchini,’’ alisema Mhe. Chande.
Mhe. Chande alifafanua kuwa mwelekeo wa Serikali ni kuifanya mifumo yote
iwe pamoja ili kupunguza wingi wa kodi, tozo na usumbufu kwa wafanyabiashara na
kuwa mifumo hiyo itakapokamilika taarifa itatolewa kwa umma.
No comments:
Post a Comment