...............................
Na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri wa Fedha, Hamad Chande
ameipongeza Benki ya Biashara ya Mkombozi,kuwa imepanda kutoka hatua moja
kwenda nyingine ndani ya muda mfupi huku amewasihi watendaji wa Benki hiyo
kutoridhika na hatua waliyofikia, badala yake waendelee kufanya uhamasishaji
ili kuifanya Mkombozi Benki iendelee kukua.
Akizungumza Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande katika Hafla ya Mkombozi
Benki kupandishwa Rasmi kutoka Soko la Ukuzaji Mitaji la DSE (EGM) na kwenda
kwenye Soko Kuu la Uwekezaji (MIMS) iliyofanyika Kambarage House jijini Dar es
Salaam.
“Hongereni sana Mkombozi Bank kwa hatua hii mliyofikia, kwa sababu mmepanda
hadhi kutoka hatua moja kwenda nyingine ndani ya muda mfupi sana. Lakini
niwaombe, msiridhike na hatua hiyo mliyoifikia, kwa sababu kuna maneno yanasema
‘Mpanda patosha, huvuna pa mkwisha.”
“Endeleeni kuhamasisha ili Bank hii ya Mkombozi iendelee kukua. Kwa hiyo
naomba kutangaza rasmi kwamba Mkombozi Bank imepandishwa rasmi kutoka Soko la
Ujasiriamali (EGM) na kuingizwa Katika Soko Kuu la Uwekezaji (MIMs),” amesema
Naibu Waziri.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Mkombozi, Respige Kimati
amesema kuwa Benki hiyo imewekeza nguvu nyingi ili kuanza kutoa gawio kwanzia
mwakani 2025, kuwa Benki hiyo imekuwa mstari wa mbele kuungana na Serikali katika
kuwashika mkono watu waliopatwa na majanga mbalimbali ndani ya jamii.
"Tumeshuhudia ukuaji mkubwa wa faida, ongezeko la amana za wateja,
ongezeko la mikopo iliyotolewa kwa watanzania hasa sekta binafsi, kupanuka kwa
mtandao wetu wa matawi na uwekezaji mzuri katika huduma za benki kwa njia ya
Mtandao, hususani uanzishwaji na usambazaji wa huduma za Benki kwa njia wa
Mawakala". amesema Kimati
Aidha, Kimati amesema Malengo ya benki hiyo ni kumkomboa Mtanzania katika
wimbi la umasikini kwa kutoa huduma za kibenki hasa mikopo midogo midogo kwa
watu binafsi wakiwemo vijana na wanawake na mikopo ya kati na mikubwa kwa
makampuni, taasisi za huduma na wafanyabiashara wa kati na wadogo.
Hivyo, hatua hii mpya ya kuwa sehemu ya Soko Kuu la Uwekezaji (MIMS) katika Soko la Hisa la Dar es Salaam, tunayo imani kubwa kwamba mafanikio zaidi yanakuja mbele yetu, tunahitaji kuendelea kupata msaada wenu wa dhati na tunawaomba washirika wetu, wateja wetu, wanahisa, mamlaka mbalimbali za usimamizi wa sekta ya fedha nchini na watunga sera kuendelea kutuunga mkono katika safari hii ili Msaada wenu ni muhimu sana katika kuhakikisha tunatimiza malengo yetu ya muda mrefu na kuboresha huduma zetu kwa wateja wetu.
Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande (wa pili) na viongozi wengine wakifurahia jambo wakati wa hafla hiyo.
No comments:
Post a Comment