ANTHONY MAVUNDE WAZIRI WA MADINI ALIEAMINIWA NA RAIS, ANAFANYA MAPINDUZI MAKUBWA SEKTA YA MADINI - UMOJA BANKING BLOG

Breaking

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, 22 September 2024

ANTHONY MAVUNDE WAZIRI WA MADINI ALIEAMINIWA NA RAIS, ANAFANYA MAPINDUZI MAKUBWA SEKTA YA MADINI

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, akizungumza katika moja ya mikutano yake na waandishi wa habari jijini Dodoma

...................................

Imeandaliwa na Dotto Mwaibale

(0754-362990)

MAENDELEO ya nchi yoyote duniani yanategemea uzalendo wa kiongozi anayeiongoza mwenye dhamira na kuwiwa kuwatumikia wananchi pasipo ya kuwabagua kisiasa, kijinsia, kiuchumi, elimu wala dini zao.


Hapa nchini tuna viongozi wengi wazalendo ambao wanaitumikia nchi kwa kujituma baada ya kuaminiwa kushika nafasi walizo nazo kupitia kada mbalimbali ikiwemo siasa.


Leo napenda kumzungumzia Anthony Peter Mavunde Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Waziri wa Madini.


Mavunde baada ya kuaminiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuteuliwa kushika nafasi hiyo kutoka Wizara ya Kilimo ambako alihudumu nafasi ya Naibu Waziri wa Kilimo anaonesha shauku kubwa ya kufanya mapinduzi makubwa ya kiuchumi kupitia madini.


Kiongozi huyu mwenye uzoefu mkubwa wa uongozi amekuja na mikakati mbalimbali ambayo inaonesha kuleta tija kwa wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa ambao wanaofuata taratibu na miongozo iliyowekwa na Wizara ya Madini.


Waziri Mavunde tangu ameteuliwa kushika nafasi hiyo amekuwa sio kiongozi wa kukaa ofisini bali amekuwa akitoka kwenda kujua changamoto za wachimbaji na kuzitafutia ufumbuzi.


Mavunde pia amekuwa akikutana na wadau mbalimbali wa sekta ya madini wa ndani na nje ya nchi kwa lengo la kubadilishana uzoefu huku dhamira yake kubwa ni kuona madini yana wanufaisha watanzania kwa kuinua uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja.


Waziri Mavunde baada ya kuteuliwe kushika nafasi hiyo jambo la kwanza alilolifanya ni kukutana na watendaji wote wa Sekta ya madini na kuzungumza nao kupanga mikakati ya kuiendeleza sekta hiyo ambayo ni jicho la nchi kwenye suala zima la uchumi.


Waziri Mavunde moja ya kazi aliyoifanya baada ya kushika nafasi hiyo ni pale alipomuelekeza Katibu Mtendaji  wa Tume ya Madini, kufuta jumla ya maombi na leseni za Utafiti 2648 ili kupisha waombaji wengine kupata fursa ya kuomba na kuendeleza maeneo hayo kwa manufaa ya Taifa na Ukuzaji wa Sekta ya Madini.

Mavunde alitoa maagizo hayo Machi 22, 2024 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ambapo alisema walikuwepo baadhi ya wamiliki wa leseni ambao walikuwa hawazingatii utekelezaji wa majukumu yao ya umiliki wa leseni kwa mujibu wa Sheria ya Madini, Sura 123.

Alisema miongoni mwa makosa ambayo yalikuwa yakijitokeza mara kwa mara ni pamoja na wamiliki wengi wa leseni kutoendeleza maeneo ya leseni zao na badala yake kuyahodhi  na kutolipa ada stahiki za leseni.

Mavunde alisema kwamba Serikali kupitia Tume ya Madini ilifuta jumla ya maombi ya leseni 227 ambayo yamekosa vigezo vya kuendelea kufanyiwa kazi. 


“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wetu. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka kipaumbele katika kuendeleza sekta ya madini nchini hivyo sisi kama Wizara ya Madini hatupo tayari kufifisha juhudi hizi njema za kiongozi wetu.” alisema Mavunde. 


Katika kuonesha kuwa na  dhamira ya dhati Tanzania imedhamiria kuwa kitovu cha uchenjuaji na uongezeaji thamani madini kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati ili kuongeza fursa za ajira na mapato kutoka na mnyororo wa thamani kwenye sekta ya madini kauli ambayo aliitoa Januari 9, 2024 akiwa jijini Riyadh, Saudi Arabia alipokuwa  akichangia kwenye mkutano wa madini wenye dhumuni la kujadili nafasi ya madini katika maendeleo ya nchi wazalishaji.


Waziri Mavunde katika kufanya maboresho ya sekta hiyo  Juni 12, 2024 alizindua Timu itakayoandaa Andiko la maudhui ya Vision 2030 huku akisisitiza kuwa Madini ni Maisha na Utajiri.


Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mavunde alisema  kuandaliwa kwa andiko hilo ni matokeo ya maelekezo aliyoyatoa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kufanyika kwa utafiti wa kina ili kuboresha eneo hilo na hatimaye kuwawezesha watanzania wasichimbe kwa kubahatisha.


Waziri Mavunde alisema kwamba, mpaka sasa utafiti wa kina kwa nchi nzima umefanyika kwa asilimia 16 ambapo mpango uliopo kupitia Vision 2030 ni kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.


Ili kwenda na kasi ya Rais Dkt.Samia ya kukuza uchumi wa nchi kupitia madini  Mavunde alilitaka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuweka mikakati madhubuti ya kukuza uwekezaji wa shirika na kulifanya kuwa kati ya mashirika makubwa katika sekta ya madini kwa bara la Afrika.


Alitoa agizo hilo Aprili 18,2024 jijini Dodoma katika kikao kilichohusisha Bodi ya Wakurugenzi ya STAMICO na Menejimenti kwa lengo la kujadili Utekelezaji wa Mipango Kazi ya Shirika kwa Mwaka wa 2023/2024.


Alisema Tanzania ni nchi iliyobarikiwa kuwa na aina mbalimbali za madini hivyo STAMICO inatakiwa kuwekeza zaidi katika utafiti wa madini ili kupata taarifa za kina zitakazowezesha ufunguzi wa migodi mikubwa ya madini badala ya kutegemea wawekezaji kutoka nje ya nchi.


Aidha Waziri wa Madini Anthony Peter Mavunde katika kuendelea kufanya maboresho kwenye sekta hiyo aliwataka Watumishi wa Wizara ya Madini kuacha kufikiri ndani ya boksi badala yake wawaze nje ya boksi kwa kuleta vitu tofauti ili kukuza Wizara kwa Ubunifu na Kushauriana na Waziri.

Ziara zake za kutembelea maeneo ya wachimbaji hasa wadogo na kusikiliza kero zao katika maeneo mbalimbali zimerudisha ari kwa wachimbaji hao na kujiona nao kuwa ni wanufaika wa rasilimali za nchi.


Baadhi ya Wachimbaji walionufaika na ziara hizo ni wa kampuni ya Green Garnet eneo la Lemshuku Kata ya Komolo wilayani Simanjiro mkoani Manyara, ambao walilalamikia  juu ya changamoto ya ukosefu wa maji, nishati ya umeme na ubovu wa barabara.


Mafanikio haya makubwa ambayo sekta ya madini inayapata kupitia Waziri Mavunde yanatokana na ushirikiano anaoupata kutoka kwa viongozi wenzake, watumishi wa wizara hiyo na wadau mbalimbali na zaidi ni kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Serikali anayoiongoza.


Mavunde Rais amekuamini endelea kuchapa kazi kwani kila mtanzania mpenda maendeleo ataungana nami katika hilo, Mungu akupe afya njema ili uendelee kulitumia Taifa kupitia wizara hiyo ya Madini. Kazi Iendelee.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, akizungumza na waandishi jijini Dodoma.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, akizungumza akiwa katika moja ya ziara zake ya kusikiliza kero za wachimbaji na kuzitafutia ufumbuzi eneo la Simanjiro mkoani Arusha.
Mkutano wa kusikiliza kero ukifanyika

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, akiwa katika ziara ya kutembelea na kukagua mgodi wa Almas wa Mwadui Shinyanga.Waziri Mavunde akiwa katika picha ya pamoja na wananchi na viongozi mbalimbali alipokwenda kusikiliza kero na kuagiza kufanyiwa marekebisho ya dosari zote za kiusalama zilizopo katika eneo la uchimbaji wa madini Mwakitolyo mkoani Shinyanga.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad

Pages