Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna
.................................
Imeandaliwa na Dotto Mwaibale (0754-362990)
KUNA usemi uliozoeleka miongoni mwa jamii kuwa mwanamke akiwezeshwa anaweza, binafsi napingana na usemi huo nakusema jitihada binafsi za mwanamke katika masomo na kufanya kazi kwa weledi zinaweza kumfikisha kwenye mafanikio tarajiwa licha ya kusaidiwa na makundi mengine ya watu wakiwemo walimu.
Hapa nataka kumuelezea Ruth Zaipuna Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Benki ya NMB ambaye kwa muda mfupi tangu ashike nafasi hiyo amefanya maboresho makubwa ya utendaji kazi ndani ya benki hiyo.
Zaipuna ni Mtanzania wa kwanza kushika nafasi hiyo ya juu katika benki hiyo iliyokuwa ikishikwa na wageni ambapo kabla yake mkurugenzi mtendaji wa benki hiyo alikuwa ni raia wa Afrika Kusini , Ineke Bussemaker.
Agosti 2020 Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya NMB ilimtangaza Zaipuna kuwa Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa benki hiyo, uteuzi ulioanza rasmi Agosti 18,2020 baada ya kutangazwa na Mwenyekiti wa Bodi ya NMB, Dkt. Edwin Mhede huku akikiri kuwa mchakato wa kumpata haukuwa mwepesi lakini hakukuwa na upendeleo isipokuwa walitazama wasifu, utendaji na maslahi ya benki na Tanzania.
Dkt. Mhede alisema katika kipindi kirefu benki hiyo ilikosa mtu baada ya aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wake kuondoka hivyo walibaki na mtu aliyekuwa anakaimu kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu lakini takwa la kisheria lilikuwa linawabana kuwa ni lazima wapate mtu.
“ Zaipuna anakuwa mtanzania wa kwanza kushika nafasi hii tangu benki hii ilipobinafsishwa ambapo kwa nyakati zote nafasi za juu zilishikwa na wageni wakiwemo Ineke Bussemaker aliyekuwa mkurugenzi tangu 2014 – 2018 kisha nafasi hiyo ikachukuliwa na Albert Jonkergow aliyeshikilia kwa kipindi cha mpito cha miezi sita kabla ya Zaipuna kupewa nafasi ya kukaimu, ” alisema Mhede.
Mwenyekiti huyo alisema mchakato wa kumpata mtendaji mkuu huyo ulikamilika Juni 30,2020 na baadaye kumtangaza huku akieleza sifa zote zilizotakiwa katika nafasi hiyo, walijiridhisha kuwa Zaipuna anazo hivyo hakukuwa na shaka kuhusu utumishi wake katika nafasi hiyo.
Mara baada ya kuanza rasmi kazi kwa nafasi hiyo jambo la kwanza alililolifanya ni kukutana na menejimenti ya benki hiyo pamoja na wafanyakazi kwa ajili ya kupanga mikakati ya ufanyaji wa kazi.
Baada ya hapo alifanya ziara ya kuwatembelea viongozi mbalimbali kwa lengo la kujitambulisha na kuona namna ya kushirikiana baina yao na benki hiyo.
Mafanikio machache aliyoyapata kwa miaka mitatu tangu ashike wadhifa huo ni kutunukiwa tuzo ya heshima ya uongozi bora wa biashara barani Afrika kwa uongozi wake shupavu wa taasisi hiyo kubwa ya fedha kuliko zote nchini Tanzania.
Zaipuna alitunukiwa tuzo hiyo maalum ya “African Business Leadership Commendation Award” ya mwaka 2022 na Jarida la African Leadership kwa juhudi zake za kuifanya Benki ya NMB kuwa mstari wa mbele kwenye ujenzi wa taifa na kuchangia kikamilifu kuboresha maisha ya watanzania.
Kujiimarisha kimataifa, Zaipuna ameweza kukutana na viongozi mbalimbali na kufanya nao mazungumzo yenye lengo la kuboresha benki hiyo akiwemo Makamu wa Rais Mwandamizi wa Mastercard Afrika Mashariki, Shehryar Ali.
Mazungumzo hayo yaliyohudhuriwa na maafisa waandamizi kutoka pande zote mbili yaliyojikita katika kujadili fursa za ubunifu wa njia rahisi za malipo ili kuharakisha ajenda ya nchi ya kuwa na uchumi wa kidijitali yalifanyika makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam.
Ndani ya nchi, Zaipuna akiambatana na Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara, Filbert Mponzi aliweza kukutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe na kumpongeza waziri huyo kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya ndani ya wizara hiyo inayoleta maendeleo makubwa kwenye sekta ya kilimo.
Mazungumzo hayo, pamoja na mambo mengine yalilenga kuimarisha ushirikiano katika kuendeleza sekta ya kilimo nchini.
Waziri Bashe alitumia nafasi hiyo kuipongeza benki hiyo kwa kuendelea kushirikiana na serikali kutoa huduma za kifedha kwa wadau wa sekta ya kilimo, ikiwemo kuongeza mikopo kutoka Sh. Bilioni 739 mwaka 2021 mpaka kufikia Trilioni 1.6 mwaka 2023, huku zaidi ya Sh. Bilioni 450 ikiwa imetolewa kwa riba nafuu isiyozidi asilimia 9 ambapo aliahidi kuendeleza ushirikiano uliopo ili kuleta tija zaidi.
Aidha, afisa mtendaji huyo alikutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba ambapo Zaipuna alielezea namna uwekezaji wao kwenye teknolojia unavyochochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini kupitia masuluhisho mbalimbali.
Hakuishia hapo, pia alielezea mchango wa NMB katika utoaji wa elimu ya fedha kwa wateja wao na jamii kwa ujumla.
Mafanikio mengine ya benki hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu ni kutoa gawio la Sh. Bilioni 30.7 kwa serikali lililopokelewa na Makamu wa Rais, Dkt Philip Isdor Mpango aliyeisifia benki hiyo na kueleza kuwa gawio hilo la Benki ya NMB ndani ya kipindi cha miaka mitano linakua na imetoa jumla ya Sh. Bilioni 80.544 kwa serikali.
Ziara za CEO Zaipuna za kutembelea kanda za benki hiyo na matawi na kukutana na wafanyakazi kisha kuzungumza nao ili kujua changamoto na kupokea maoni yao na kuyafanyia kazi ni moja ya njia inayosaidia kufanya maboresho ya kiutendaji.
WADAU MBALIMBALI WANAMZUNGUMZIAJE CEO ZAIPUNA ?
Hawa Omari mkazi wa Majimatitu Mbagala jijini Dar es Salaam
anasema mara nyingi viongozi wanawake katika maeneo mengi ambayo wamekuwa
wakiaminiwa wanafanya kazi vizuri tena kwa hofu ya Mungu tofauti na baadhi ya wanaume.
Grace Mwakasege mtumishi wa benki hiyo anasema hivi imepiga
hatua mara dufu tofauti na wakati ule ilipokuwa ikiongozwa na wageni kutoka
nje.
“Ni seme tu kuwa Benki ya NMB sasa tupo mbele zaidi
kimaendeleo,” alisema Mwakasege.
Kwa upande wake mbobezi wa masuala ya kiuchumi ambaye pia ni
Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (TAA), Profesa Eliamani Sedoyeka anasema kihistoria wanawake wanauwezo
mkubwa sana hasa kwa kusimamia majukumu mengi.
Tangu wakiwa watoto ukiangalia makuzi yao mtoto wa kike hasa
nchi za kiafrika utaona majukumu mengi wakipewa wao yale ya kawaida nyumbani
kama kuchota maji, kupika na kuwalea wadogo zake.
Alisema kwa muktadha huo wamekuwa wakijengwa na jamii ambapo
ukimkuta mtoto wa kike ambaye familia yake imelitambua hilo na kumsomesha na
kumuendeleza moja kwa moja anakuja kuwa na mchango mkubwa sana katika jamii.
“Ukimkabidhi mwanamke jukumu wengi wao wanakuwa na hofu ya
kuharibu kwa hiyo wanaweka nguvu kubwa na kuhakikisha mambo yanakwenda sawa,”
alisema
Alisema nchini Uingereza
hadi mwaka jana karibiria selusi mbili ya mameneja ni wanawake ni
mabadiliko yanayotokea duniani ya kuwapa nafasi wakina mama kwa kuwa
hawatuangushi na wamekuwa wakifanya vizuri kama alivyo huyu CEO wa Benki ya
NMB.
Kwa sisi tunaona ni hatua kubwa na nzuri ya kupendeza na
kama kitaifa tumeonesha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyoachiwa nchi na kufanya vizuri sana.
“Mwanamke kukabidhiwa nchi baada ya kifo cha Magufuli tumeona alivyofanya kazi kubwa ni jambo la kujivumia sana,” alisema.
Mwalimu Willy Sumia mkazi wa Sumbawanga mjini mkoani Rukwa anasema taaisi yoyote ya fedha ikimpata kiongozi wa kuisimamia vizuri na kufanya maboresho makubwa ya kiubunifu mambo yana kwenda sawa.
“Tangu uanze utaratibu ulioanzishwa na Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu wa kutoa magawio kwa wazi chini ya CEO Zaipuna tumeshuhudia jinsi benki hiyo ambavyo inatoa kiasi kikubwa cha fedha ni jambo ambalo watanzania tunapaswa kujivunia.
Alisema fedha hizo ndizo zinatumiwa na Serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali na kulipa mishahara ya watumishi wake.
Mohamed Mambo Mkazi wa Tunduru mkoani Ruvuma anasema Benki hiyo kumpata CEO wa kwanza mzawa tena mwanamke inaonesha jinsi kundi la wanawake lilivyo na umuhimu hasa katika kuchagiza maendeleo na kuondoa dhana na mfumo dume uliokuwa umezoeleka zamani kuwa wakuu wa taasisi kubwa ni lazima wawe wanaume.
Mjasiriamali katika soko la Vitunguu la Kitaifa lililopo eneo la Misuna Manispaa ya Singida, Aisha Muna anasema chini ya Afisa Mtendaji huyo wa NMB wanafurahia mikopo mbalimbali wanayokopeshwa baada ya kukidhi vigezo kwa kujiunga katika vikundi.
:"Afisa Mtedaji Mkuu (CEO) wa Benki ya NMB, Zaipuna kwa muda
muda mfupi tangu ashike nafasi hiyo ameonesha njia na kuthibitisha wanawake
wakiaminiwa wanawezakufanya makubwa,” alisema Aisha.
Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (katikati) na maofisa wengine wa benki hiyo wakionesha tuzo tatu za kutambuliwa kimataifa iliyotunikiwa benki hiyo.
Tuzo hizo tatu ni Benki Bora Tanzania 2023 (Kutoka Tuzo za Umahiri za EuroMoney), Benki Bora ya Wateja Maalum (Kutoka Tuzo za Umahiri za EuroMoney) na Benki Bora ya Wateja Binafsi na Biashara (Kutoka Tuzo za Global Banking and Finance Review)
Tuzo hizo zimetolewa na majarida ya kimataifa yenye makao makuu
yake London, Uingereza – na leo Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi. Ruth Zaipuna
amezitambulisha rasmi katika hafla fupi iliyofanyika katika ofisi za Makao
Makuu ya NMB.
“Hii ni mara ya 10 Benki ya NMB kutambulika kama Benki Bora nchini
ndani ya miaka 11 iliyopita, ikidhihirisha ufanisi wetu wa kiutendaji,
mapinduzi ya kiteknolojia na ubunifu, uongozi dhabiti, na uimara wetu katika
kuleta masuluhisho yanayomgusa kila Mtanzania,” anasema Bi. Ruth Zaipuna.
“Tunawashukuru wateja wetu, wanahisa, wafanyakazi, Benki Kuu,
Serikali pamoja na wadau wetu wote kwa kuendelea kutuamini na kutufanya kuwa
Benki Bora nchini,” amesema.
Endeleeni kufurahia huduma za Benki ya NMB, kwani # HapaNdioNyumbani.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango (wapili toka kulia) akipokea mfano wa hundi
yenye thamani ya zaidi ya Sh.Bilioni 30.7 kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa
Benki ya NMB – Ruth Zaipuna (watatu toka kulia) ikiwa ni gawio kwa Serikali
katika hafla iliyofanyika Jijini Dodoma. Wengine ni Waziri wa Fedha na
Mipango ,Mhe.Dkt.Mwigulu Nchemba(wa pili kulia), Afisa Mkuu wa Fedha
NMB(kushoto), Juma Kimori na wapili toka kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Benki
ya NMB, Dkt. Edwin Mhede.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi. Ruth Zaipuna alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe.
No comments:
Post a Comment