“Maendeleo tunayoyaona nchini kwetu katika kila sekta yanategemea mchango
wa Serikali pamoja na sekta binafsi. Dhamira na maono ya Rais wetu, Dkt. Samia
Suluhu Hassan ni kuimarisha sekta binafsi ili ihuishwe na kuwa mshindani katika
kuleta maendeleo makubwa kwa nchi yetu,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana usiku (Jumanne, Julai 23, 2024) wakati
akizungumza na wadau wa sekta binafsi nchini kwenye ufunguzi wa maadhimisho ya
Wiki ya Sekta Binafsi Tanzania kwa mwaka 2024 yaliyofanyika Super Dome, Masaki,
jijini Dar es Salaam.
Wiki ya Sekta Binafsi Tanzania inaenda sambamba na maadhimisho ya miaka 25
ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).
Amezitaka wizara na taasisi za Serikali ziendelee kupokea maoni ya sekta
binafsi na kuhakikisha yanazingatiwa katika marekebisho ya sera na sheria za
biashara ili kuondoa vikwazo vya urasimu na kuboresha taratibu za usajili na
uendeshaji wa biashara nchini kwa kuwezesha upatikanaji wa vibali na leseni kwa
haraka na kwa urahisi.
Pia amezitaka wizara zinazohusika na viwanda, biashara na uwekezaji
zihakikishe zinabuni mbinu za kukuza na kusaidia biashara ndogo na za kati
(SMEs). “Wekeni mazingira mazuri ya upatikanaji wa mikopo nafuu, mafunzo na
ufikiaji wa masoko ili kusaidia biashara ndogo na za kati kukua na kuchangia
katika uchumi. Biashara hizi ni sehemu muhimu ya kuimarisha sekta binafsi.”
Akielezea jitihada ambazo zimechukuliwa ili kukuza sekta binafsi na
uwekezaji, Waziri Mkuu amesema Serikali imeimarisha mazingira ya biashara kwa
kufanya marekebisho katika sera na sheria za biashara ili kuondoa vikwazo
vinavyowakabili wafanyabiashara na wawekezaji.
“Hatua hizi zimejumuisha kuboresha taratibu za usajili wa biashara,
kupunguza urasimu, na kuongeza uwazi, kutoa fursa za uwekezaji katika sekta
mbalimbali kama vile kilimo, nishati, miundombinu, utalii, viwanda na kuanzisha
maeneo maalum ya uwekezaji.”
Amesema Serikali imewekeza katika miundombinu ya usafirishaji, nishati,
maji na mawasiliano ambayo ni muhimu kwa shughuli za uwekezaji na biashara.
“Hatua hii inalenga kuimarisha mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji wa
ndani na nje,” amesema.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzugumza na washiriki wa hafla hiyo,
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Jenista
Mhagama amempongeza Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kuasisi falsafa mpya ya kushirikiana na Sekta
binafsi ikiwemo kuondoa ukiritimba wa mawazo.
“Rais wetu yeye anaamini na anakiri katika dhana ya kusikiliza sauti na
mawazo ya wengine ili kuweka mazingira bora ya mahusiano kati ya Sekta binafsi
na Serikali”
Amesema kuwa kupitia falsafa hiyo imeshuhudiwa Rais Dkt. Samia akiendesha
vikao vya kubadilishana mawazo mara kwa mara na makundi tofauti ya sekta
binafsi yaliyojikita katika sekta mbalimbali kwa kusikiliza changamoto,
kujifunza mafanikio na kutengeneza mfumo thabiti na sahihi wa kusonga mbele kwa
manufaa ya pande zote mbili
Naye, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe alisema katika
mwaka huu wa fedha, wizara hiyo imeweka vipaumbele sita ambavyo vinalenga kuboresha
mazingira ya ufanyaji biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Kwa upande wake, Mweyekiti wa TPSF, Angelia Ngalula, alisema kuwa
wanatamani kuona Tanzania inakuwa kitovu cha Afrika kutokana na rasilmali
ilizonazo. “Pia tunatamani kuona biashara nyingi zinarasimishwa na wigo wa
walipakodi unaongezwa,” alisema.
Alisema wakati TPSF inaanzishwa, ilikuwa na wanachama 33 lakini kwa sasa
imefikisha wanachama zaidi ya 500 ambao wanajumuisha vyama vya wafanyabiashara
na makampuni makubwa.
No comments:
Post a Comment