Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
maendeleo yaliyopo nchini hivi sasa yametokana na uhusiano mzuri uliopo baina
ya Serikali na sekta binafsi.
“Maendeleo tunayoyaona nchini kwetu
katika kila sekta yanategemea mchango wa Serikali pamoja na sekta binafsi.
Dhamira na maono ya Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuimarisha sekta
binafsi ili ihuishwe na kuwa mshindani katika kuleta maendeleo makubwa kwa nchi
yetu,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Julai 23,
2024 wakati akizungumza na wadau wa sekta binafsi nchini kwenye ufunguzi wa
maadhimisho ya Wiki ya Sekta Binafsi Tanzania kwa mwaka 2024 yaliyofanyika
Super Dome, Masaki, jijini Dar es Salaam.
Wiki ya Sekta Binafsi Tanzania inaenda
sambamba na maadhimisho ya miaka 25 ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania
(TPSF).
Amezitaka wizara na taasisi za Serikali
ziendelee kupokea maoni ya sekta binafsi na kuhakikisha yanazingatiwa katika
marekebisho ya sera na sheria za biashara ili kuondoa vikwazo vya urasimu na
kuboresha taratibu za usajili na uendeshaji wa biashara nchini kwa kuwezesha
upatikanaji wa vibali na leseni kwa haraka na kwa urahisi.
Pia amezitaka wizara zinazohusika na
viwanda, biashara na uwekezaji zihakikishe zinabuni mbinu za kukuza na kusaidia
biashara ndogo na za kati (SMEs). “Wekeni mazingira mazuri ya upatikanaji wa
mikopo nafuu, mafunzo na ufikiaji wa masoko ili kusaidia biashara ndogo na za
kati kukua na kuchangia katika uchumi. Biashara hizi ni sehemu muhimu ya
kuimarisha sekta binafsi.”
Akielezea jitihada ambazo zimechukuliwa
ili kukuza sekta binafsi na uwekezaji, Waziri Mkuu amesema Serikali imeimarisha
mazingira ya biashara kwa kufanya marekebisho katika sera na sheria za biashara
ili kuondoa vikwazo vinavyowakabili wafanyabiashara na wawekezaji.
Mfanyabiashara Haidary Gulamali
akizungumza katika maadhimisho hayo alisema licha ya kuzalisha magodoro ya Dodoma
Asili pia wanazalisha mafuta ya alizeti ambayo uzalishaji wake kwa siku ni tani
100 na kuwa kiwanda hicho kipo Dodoma.
Alisema kiwanda hicho kimetoa ajili 1000
na wakulima wamepata fursa ya kuuza alizeti katika kiwanda hicho ambapo
alihimiza wananchi waendelee kutumia mafuta hayo bora kwa matumizi ya kupikia vyakula vyao.
Gulamali alimshukuru Rais Samia Suluhu
Hassan kwa kutoa fursa ya kufanya
biashara kwani kampuni yao pia inafanya
biashara ya kuagiza vibiriti aina ya kasuku
kutoka nchini Kenya baada ya
kufanya ziara ya kikazi nchini humo.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu na kuomba
mfikishie salamu zangu Rais Samia kuwa vibiriti hivi vya kasuku si kwa ajili ya
kuwashia jiko tu bali inakwenda kuwasha moto wa miaka mitano mingine tena kwake
na kuhakikisha moto huo hautazimika hadi anaingia Ikulu,” alisema Gulamali huku
akishangiliwa.
Alisema kwa jitihada za Rais Samia na
TPSF waliweza kufanya ziara ya kutembelea Indonesia na wao wakiwa miongoni mwao
ambapo alifanikiwa kuleta sabuni ya mche ambayo ameipa jina Gulamali na
amehimiza wananchi kudumisha usafi kwa kutumia sabuni hiyo.
Gulamali alisema ziara nyingine kama hiyo
waliifanya na Rais Samia nchini Norway ambapo walikutana na wafanyabiasha wa
nchi hiyo ambapo kampuni yake imeweza kuleta maziwa aina ya Dutch Lady ambayo
tayari yapo sokoni hapa nchini na yanachangamkiwa na watanzania pamoja na
watalii, bidhaa hiyo ilikuwa ikipatikana katika nchi zao lakini leo hii
inapatikana hapa kwetu.
Aidha, Gulamali akisema watanzania wakithubutu wanaweza kwani yeye kupitia kampuni yake ya Gulamali Group of Company wameweza na akatumia nafasi hiyo kuwahimiza wafanyabiasha kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchini.
No comments:
Post a Comment