Na Mwandishi Wetu
Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha), Bi. Sauda Msemo, amewaasa viongozi wa kike wa mabenki kuandaa na kutekeleza programu na mikakati itakayopunguza pengo la kijinsia kati ya wanaume na wanawake katika umiliki wa akaunti za Benki.
Naibu Gavana ameyasema hayo katika mkutano na viongozi hao ambao ulilenga kujadili namna ya kuboresha huduma na bidhaa za kifedha zinazolenga wanawake nchini ili kuongeza ujumuishwaji wa wanawake katika sekta hiyo.
Aidha, ametaja uhaba wa elimu ya fedha, kukosekana kwa taarifa sahihi za wanaume na wanawake wanaotumia huduma za fedha (Gender Disaggregated Data) na sababu za kiutamaduni na hali duni ya kiuchumi kuwa miongoni mwa visababishi vya kuwepo kwa pengo hilo.
Pia, amewapongeza viongozi hao kwa kuendelea kufanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha wanawake wanafikiwa na wanatumia huduma mbalimbali za kifedha.
Ripoti ya FinScope ya Mwaka 2023 inaonesha asilimia 18 ya wanawake wana akaunti katika benki ukilinganisha na asilimia 27 ya wanaume.
No comments:
Post a Comment