Waziri wa Fedha, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (Kulia), akiagana na Balozi wa Denmark nchini Tanzania aliyemaliza muda wake, Mhe. Mette Dissing-Spandet, baada ya kikao chao kilichofanyika katika Ofisi za Hazina Ndogo, jijini Dar es Salaam, ambapo ameiomba Denmark kuongeza ushirikiano katika sekta za nishati, maendeleo ya sekta ya fedha na kukuza uwekezaji, katika mpango wao mpya wa ushirikiano wa kimataifa unaoandaliwa na nchi hiyo.
..............................
Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
WAZIRI wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameishauri Denmark
kuongeza masuala ya ushirikiano katika sekta za nishati, maendeleo ya sekta ya
fedha na kukuza uwekezaji katika mpango wao mpya wa ushirikiano wa kimataifa
unaoandaliwa na nchi hiyo.
Dkt. Nchemba ametoa rai hiyo wakati akimuaga Balozi wa Denmark nchini
Tanzania aliyemaliza muda wake, Mhe. Mette Dissing-Spandet, katika Ofisi za
Hazina Ndogo, Jijini Dar es Salaam.
Katika kikao hicho, Dkt. Nchemba alimshukuru Balozi Dissing-Spandet kwa kufanikisha
kusitishwa kwa uamuzi uliotaka kuchukuliwa na nchi yake wa kufunga ubalozi wake
hapa nchini na kwa kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya Tanzania na Denmark.
Aidha, Dkt. Nchemba alisema kuwa mchango wa Denmark katika maendeleo ya
nchi umekuwa mkubwa katika Nyanja mbalimbali ikiwemo ujenzi wa reli ya SGR,
sekta ya afya, utawala bora, kukuza ajira, demokrasia, utawala wa sheria na
haki za binadamu, miradi ambayo alisema inachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza
umasikini wa wananchi.
Alimwomba Balozi huyo kuwa balozi mzuri wa Tanzania katika kuhamasisha
kampuni za Denmark kuja kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali za kiuchumi
ikiwemo ujenzi wa viwanda vya kuzalisha mbolea na miradi ya nishati kwa njia ya
upepo.
Kwa upande wake Balozi wa Denmark nchini Tanzania aliyemaliza muda wake,
Mhe. Mette Dissing-Spandet, alisema kuwa anajivunia mafanikio makubwa
yaliyopatikana katika kipindi cha uwakilishi wake hapa nchini ambapo
ameshuhudia nchi ikipiga hatua kubwa kiuchumi na kijamii.
Aliahidi kuwa ataendelea kuwa balozi mzuri wa Tanzania ili kuvutia
uwekezaji na kwamba kampuni nyingi za nchi yake zimeonesha nia ya kuwekeza hapa
nchini.
Alisema kuwa alama kubwa anayoiacha ni pamoja na kuishawishi nchi yake kuachana na mpango wa kufunga shghuli za kibalozi hapa nchini na kwamba hatua hiyo itaiwezesha Denmark kujipanga upya na kuja na mpango mkubwa wa kushirikiana na Serikali katika kukuza maendeleo ya nchi.Waziri wa Fedha, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akizungumza wakati wa kikao na Balozi wa Denmark nchini Tanzania aliyemaliza muda wake, Mhe. Mette Dissing-Spandet (Hayupo pichani), katika Ofisi za Hazina Ndogo, jijini Dar es Salaam, ambapo ameiomba nchi hiyo kuongeza ushirikiano katika sekta za nishati, maendeleo ya sekta ya fedha na kukuza uwekezaji, katika mpango wao mpya wa ushirikiano wa kimataifa unaoandaliwa na nchi hiyo.Balozi wa Denmark nchini Tanzania aliyemaliza muda wake, Mhe. Mette Dissing-Spandet, akizungumza wakati wa kikao na Waziri wa Fedha, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (hayupo pichani), alipofika kumuaga katika Ofisi za Hazina Ndogo, jijini Dar es Salaam, ambapo Mhe. Dkt. Nchemba amewaomba kuongeza ushirikiano katika sekta za nishati, maendeleo ya sekta ya fedha na kukuza uwekezaji, katika mpango wao mpya wa ushirikiano wa kimataifa unaoandaliwa na Denmark
No comments:
Post a Comment