........................................
Na Mwandishi Wetu
WANANCHI Mkoa wa Simiyu wametakiwa kuendelea kujitokeza kwa wingi kupata
elimu ya fedha kutoka kwa wataalamu kutoka Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na kutumia elimu
watakayoipata kukuza uchumi wa Mkoa huo na Taifa kwa ujumla.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Kenani Kihongosi,
Ofisini kwake, alipotembelewa na Timu ya wataalamu wa kutoa elimu ya fedha
kutoka Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kabla
ya wataalamu hao kuelekea Wilayani Itilima Mkoani Simiyu kutoa elimu ya fedha
kwa wafanyabiashara, wajasiriamali na wananchi wa Wilaya hiyo.
‘’Niwasisitize na kuwaomba wananchi wetu wapokee mpango huu kwa sababau ni
mpango utakaowasaidia wao kujua matumizi sahihi ya fedha zao na namna bora ya
kuchukua, kutumia mikopo na kufahamu mikataba namna gani mikopo wanayochukua
inaweza kuwanufaisha katika maisha yao” Alisema Bw. Kihongosi.
Aliongeza kuwa kauli mbiu ya kampeni hiyo isemayo ‘’Elimu ya Fedha ni
Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi’’ ni muafaka kwa kuwa maendeleo ya kiuchumi lazima yatokane na
mipango thabiti na mikakati bora ya elimu ya matumizi sahihi ya fedha hasa kwa
wananchi.
Bw. Kihongosi, aliipongeza Wizara ya Fedha kwa kuandaa mpango wa maendeleo
ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya fedha nchi nzima na kuufikia Mkoa wake kutokana na umuhimu wa
elimu hiyo katika kukuza uchumi wa nchi.
‘’Niwapongeze, Wizara ya Fedha kwa kuja na mpango huu mkakati mzuri kabisa
wa kuelimisha wananchi wetu kwa sababu ni imani yetu wananchi wakipata uelewa
kuhusu masuala ya kifedha watafanya mambo mazuri yatayowasaidia kuleta tija
kiuchumi’’ Alisema Bw. kihongosi.
Akitoa ufafanuzi kuhusu sifa za kukopa baada ya mmoja ya washiriki wa
mafunzo ya elimu ya fedha katika Halmashauri ya Wilaya ya Itilima Bw. Alex
Elias kutaka kufahamu kuhusu suala la kukosa mkopo kutokana na umri kuwa
mkubwa, Afisa Mkuu Mwandamizi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bi. Mwile
Kauzeni, alisema suala la mikopo ni haki ya watu wote wenye uwezo wa kulipa
mikopo hiyo isipokuwa watoto.
‘’ Kuna taasisi moja inayoangalia taarifa za watu wote wanaokopa katika
taasisi zote Tanzania, inaitwa Credit Info, hawa watu kila mtoa huduma ameambiwa apeleke majina ya watu
wake ambao wamekopa sasa jina lako likipelekwa kule wanaona kwamba kumbe fulani
amekopa mahali pengi, je anakopesheka tena? lakini ili mtu aweze kukopa ni yeye
mwenyewe kuwa na uwezo wa kuingiza kiasi gani kila mwezi” alifafanua Bi.
Kauzeni.
Naye Afisa Usimamizi wa Fedha, kutoka Wizara ya Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Bi. Elizabeth Mnzava, alisema Timu hiyo ya wataalamu wa kutoa elimu ya fedha kutoka Wizara ya Fedha inaendelea kutoa elimu hiyo katika Wilaya za Mkoa wa Simiyu ikiwemo Busega na Meatu ambapo baada ya kukamilisha Wilaya hizo wataalamu hao wataelekea Mkoani Shinyanga kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa Mkoa wa huo.
No comments:
Post a Comment