Kamishna wa Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Dkt. Charles Mwamaja (katikati) akifurahia uzinduzi rasmi wa kampuni tanzu ya Benki ya CRDB inayotoa huduma za bima ‘CRDB Insurance Company (CIC) Ltd’ katika hafla iliyofanyika hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam 18 Juni 2024. Wengine pichani Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA), Dkt. Baghayo Saqware (wapili kulia), Afisa Mtendaji Mkuu wa Kundi la Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (wakwanza kushoto), Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi CIC, Omary Mwaimu (wakwanza kulia), na Mkurugenzi Mtendaji wa CIC, Wilson Mnzava.
---
Dar es Salaam. Tarehe 18 Juni 2024: Kamishna wa Uendelezaji wa Sekta ya Fedha nchini, Dkt. Charles Mwamaja ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuanzisha kampuni tanzu ya bima ya ‘CRDB Insurance Company (CIC)’ ambapo amesema itasaidia kwa kiasi kikubwa kuchangia ufikiaji wa malengo ya serikali ya kuongeza ujumuishi wa bima kufikia asilimia 50 kwa Watanzania weny eumri wa kuanzia miaka 18 ifikapo mwaka 2030.
Dkt. Mwamaja ameyasema hayo alipoizindua kampuni hiyo jijini hapa ukiwa umepita mwaka mmoja tangu ipate leseni ya kutoa huduma za bima zisizo za maisha kwa Watanzania ili kuwalinda dhidi ya majanga yanayoweza kujitokeza. Dkt. Mwamaja ameitaka CIC kutumia uzoefu na wigo mpana wa Benki ya CRDB kuwafikia wananchi hasa kwa kuzingatia kuwa Benki hiyo imeenea katika halmashauri zote nchini.
Dkt. Mwamaja ambaye amemwakilisha Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema sekta ya bima nchini bado ni changa lakini ina fursa kubwa sana za kuwahudumia Watanzania iwapo elimu itatolewa na makampuni ya bima kuwekeza katika ubunifu wa bidhaa zitakazogusa makundi mbalimbali ya wateja, Taifa litafikia lengo lake la kuongeza ujumuishi wa bima ifikapo mwaka 2030.
“Niwapongeze kwa ubunifu ambao mmeanza nao kwa kuja na bima ya kilimo kwa kushirikiana na ACRE Africa. Kilimo ni sekta muhimu katika uchumi wetu inayoajiri watu wengi zaidi. Iwapo mtafika mpaka vijijini mtatoa nafuu kwa wakulima wengi kulinda mazao na mifugo yao jambo ambalo litasaidia kuwapa utulivu wa nafsi a wakulima kupitia bima hii. Tunapaswa kujua kuwa huduma bora bima ni msingi wa ustawi wa uchumi na kichocheo cha uwekezaji,” amesema Dkt. Mwamaja.
Kwa upande wake Kamishna wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Dkt. Baghayo Saqware ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuwa taasisi ya kwanza fedha nchini kuanzisha kampuni tanzu ya bima. Dkt. Saqware amesema CIC inakwenda kuitanua sekta ya bima nchini jambo litakaloongeza ushiriki wa Watanzania katika kutumia huduma za bima.
Akieleza ujumuishi wa huduma za bima nchini, Dkt. Saqware amesema hadi mwishoni mwa mwaka 2023 kulikuwa na watumiaji wa bima milioni 12 kutoka watu milioni 6 waliokuwa wanatumia bidhaa hizo mwaka 2022. Dkt. Saqware amesema kupitia jitihada zinazotekelezwa na Serikali ikiwamo kuanzishwa kwa kanuni ya bima za lazima kunatarajiwa kuongeza ujumuishi mara dufu kila mwaka kufikia lengo lililowekwa.
“Serikali pia imeanzisha konsotia ya bima ya mafuta na gesi, pamoja ya ile ya kilimo na mifugo. Ni imani yangu kuwepo kwa makampuni kama CIC kutasaidia kufanikisha malengo kwa kuwekeza mitaji ili sehemu kubwa ya ada za bima ziwe zinabaki nchini,” alisema Kamishna Saqware huku akiitaka kampuni hiyo kuwekeza katika weledi kwa wafanyakazi na kusimamia sera na misingi iliyowekwa kisheria ili kuepukana na udanganyifu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Omary Mwaimu amemwambia Dkt. Mwamaja kuwa lengo walilonalo ni kuifanya CIC kuwa kampuni ya bima chaguo nambari moja kwa Watanzania wote kupitia huduma bunifu na nafuu ambazo zitatoa fursa kwa makundi mbalimbali ya wananchi kujiunga na hivyo kuchochea ujumuishi wa bima nchini.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema kuanzishwa kwa CIC ni mwendelezo wa utekelezaji wa azma ya Benki ya CRDB kutanua wigo wake wa kufikisha huduma za fedha ikiwamo bima kwa Watanzania.
Nsekela amebainisha kuwa uamuzi huo umetokana na hali ya ufikiaji mdogo wa huduma za bima nchini huku akieleza kuwa mkazo mkubwa wa kampuni hiyo ya CIC umeelekezwa vijijini ambapo wengi wapo nje ya mfumo rasmi wa bima.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa CIC, Wilson Mnzava amewakaribisha mawakala na madalali wa bima, wateja, pamoja na wadau wengine kuzitumia huduma za CIC akiahidi kuwa watapata utulivu wa maisha, utulivu wa nafsi, utulivu wa biashara, na utulivu wa uchumi wao kipindi majanga yanapojitokeza.CRDB Insurance Company (CIC) inakuwa kampuni tanzu ya nne ya Benki ya CRDB baada ya zile za CRDB Bank Burundi, CRDB Bank DR Congo, na CRDB Bank Foundation. CIC inatoa huduma za bima zisizo za maisha ikiwamo bima ya magari, bima ya nyumba, bima ya vyombo vya moto, bima ya biashara, bima ya usafirishaji, bima ya safari, bima ya ukandarasi, na bima ya mitambo.
Mkutano ukiendelea.
Mkutano ukiendelea.
Pivha ya pamoja.
Picha ya pamoja.
No comments:
Post a Comment