TANZANIA YAANDIKA HISTORIA MPYA: MFUMO WA KIBENKI WA KITAIFA WABUNIWA NA WATAALAMU WA NDANI - UMOJA BANKING BLOG

Breaking

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, 31 July 2025

TANZANIA YAANDIKA HISTORIA MPYA: MFUMO WA KIBENKI WA KITAIFA WABUNIWA NA WATAALAMU WA NDANI

Katika kile kinachoonekana kuwa hatua ya kihistoria na mfano wa kuigwa kwa bara la Afrika, Tanzania imeweka alama isiyofutika kwa kuzindua Mfumo wa Kibenki wa Kitaifa uliojumuishwa (Integrated Core Banking System - ICBS), ambao umetengenezwa kikamilifu na wataalamu wa Kitanzania kwa gharama ya Shilingi Bilioni 10.63 pekee. Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam ukiongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, ambaye ameuelezea mradi huo kuwa ni "ushindi wa kitaifa" na uthibitisho wa uwezo wa Watanzania katika ubunifu wa kiteknolojia.


UBUNIFU WA NDANI: KIELELEZO CHA KUJITEGEMEA KITEKNOLOJIA

Katika enzi ambazo mataifa mengi hutegemea mifumo ya teknolojia kutoka nje, Tanzania imesimama imara na kuonyesha kuwa uwezo wa ndani unaweza kuaminika, kuaminiwa na hatimaye kuzalisha bidhaa za kimkakati kama ICBS. Mfumo huo wa kibenki, unaotarajiwa kuongeza ufanisi, uwazi, na usalama wa taarifa za kifedha katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), umetajwa kuwa wa kipekee Barani Afrika.

Kwa mujibu wa Dkt. Mpango, mfumo huo si tu unarahisisha uchakataji wa miamala ya kifedha ya serikali, bali pia unaimarisha usimamizi wa sera za fedha, ukijumuisha taarifa muhimu za mabenki, mitandao ya fedha na taasisi za fedha zisizo za kibenki.

 “Huu ni uthibitisho kuwa tunaweza. Tuache kasumba ya kuamini kuwa kila kitu lazima kiingie kutoka nje. Tanzania ina ubongo. Na huu ndio muda wa kuuweka kazini,” alisisitiza Dkt. Mpango kwa msisitizo.

USALAMA NA UANGALIZI KATIKA ENZI ZA UHALIFU WA MTANDAO

Makamu wa Rais amebainisha kuwa ICBS imejengwa kwa misingi imara ya kiusalama dhidi ya mashambulizi ya kimtandao, jambo ambalo linaipa Tanzania nafasi ya kuwa kiongozi wa mapambano dhidi ya uhalifu wa fedha unaokithiri ulimwenguni. Ameitaka BoT kuhakikisha mfumo huo unapata hakimiliki rasmi, na kuusajili kitaifa na kimataifa, ili kulinda ubunifu huo usiweze kuibwa au kuigwa bila ridhaa ya Tanzania.

ELIMU YA FEDHA NA UKOMO WA UKOPESHAJI HOLELA

Katika hatua ya kuoanisha maendeleo ya kiteknolojia na mabadiliko ya kitabia kwa wananchi, Dkt. Mpango ametoa agizo maalum kwa Benki Kuu kutoa elimu ya fedha kwa Watanzania, haswa katika matumizi ya mikopo. Ameonya kuhusu tabia ya watu kukopa kwa ajili ya starehe, badala ya matumizi yenye tija kiuchumi. Ameitaka BoT kuhakikisha inashughulikia ukopeshaji holela unaofanywa na baadhi ya majukwaa ya mitandao, ambayo mara nyingi huwakandamiza wateja na kuleta athari za kifamilia na kijamii.

 “Tusiweke mfumo mzuri kisha tukauharibu kwa kutorudisha maadili ya kifedha kwa jamii. Elimu ni ufunguo wa kuhakikisha kuwa ICBS inaleta mabadiliko ya kweli kwenye maisha ya watu,” aliongeza.

TANZANIA YAPAA KIUCHUMI KUPITIA AKIBA YA DHAHABU

Katika hatua nyingine ya kushangaza ulimwengu wa kifedha, Dkt. Mpango alitangaza kuwa Tanzania imefanikiwa kujiweka kwenye ramani ya kimataifa kwa kuwa miongoni mwa nchi zenye akiba ya dhahabu kubwa, baada ya kununua tani 6.8 za dhahabu safi zenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 731 hadi kufikia Julai 29, 2025.

Hatua hiyo ni ya kimkakati, ikilenga kulinda thamani ya sarafu ya taifa, kuimarisha akiba ya fedha za kigeni, na kupunguza utegemezi wa fedha bandia kwenye mzunguko wa kiuchumi.

 “Tuna dhahabu siyo tu ardhini bali sasa iko na sisi kwenye hifadhi ya kitaifa. Hii ni hatua ya kipekee na inapaswa kutunzwa na kuendelezwa,” alifafanua Makamu wa Rais kwa fahari.

MABORESHO YA KITAASISI: MAKTABA NA MAKUMBUSHO YA BoT

Katika kilele cha hafla hiyo, Makamu wa Rais alizindua pia maktaba na makumbusho ya Benki Kuu, ambayo ni hazina ya maarifa kwa vizazi vya sasa na vijavyo. Amehimiza wananchi, hasa vijana na watafiti, kutumia rasilimali hiyo kuongeza maarifa ya kifedha, historia ya benki na mienendo ya sera za kiuchumi.

“Hatuwezi kuwa taifa la viwanda au la kidijitali bila kujenga jamii yenye maarifa. Maktaba hii ni chombo cha kuendeleza kizazi cha wanaofikiri mbele,” alisema kwa msisitizo.

HITIMISHO: HII NI NCHI INAYOJIAMINI

Uzinduzi wa mfumo wa ICBS umeashiria Tanzania mpya—nchi inayojiamini, inayotambua uwezo wake, na inayowekeza katika mustakabali wa kizazi kijacho. Mfumo huu unapaswa kuwa chachu ya mageuzi katika taasisi zote za umma na binafsi, ukibeba mafunzo kuwa maendeleo hayaletiwi, bali yanaletwa na juhudi, maarifa na mshikamano wa kitaifa.

Tanzania sasa inatakiwa kulinda alichokianzisha kwa kuhakikisha:

Sheria za hakimiliki zinalindwa kikamilifu.

Elimu ya fedha inafika kwa kila Mtanzania.

Mfumo huu unaboreshwa kila wakati ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia duniani.

Kwa hatua kama hizi, Tanzania si tu kwamba inajenga uchumi wa kisasa, bali pia inajenga taifa la hadhi ya kimataifa lenye msingi wa maarifa, usalama wa fedha, na uthubutu wa ndani.



Makala haya yameandikwa na Victor Bariety 0757-856284

 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad

Pages