Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
BENKI ya NMB kwa kushirikiana na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), wamezindua mashirikiano ya kimkakati na ya Kidijitali ya Ununuzi na Uuzaji wa Hisa za Kampuni mbalimbali zilizoorodheshwa DSE ambapo kupitia aplikesheni ya NMB mkononi unaeza kuipata huduma ya uuzaji na ununuzi wa hisa ya DSE.
Mashirikiano haya ni matokeo ya ubunifu na ushirikiano wa muda mrefu kati ya NMB na DSE, uliounganisha rasmi mifumo miwili ya suluhishi za kidijitali za NMB Mkononi ya Benki ya NMB na Hisa Kiganjani ya Soko la Hisa Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika leo jijini Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi Ruth Zaipuna, alisema wanajivunia mashirikiano mema na DSE, yaliyozaa huduma hiyo inayowapa Watanzania na Wawekezaji wengine njia rahisi, salama na za kisasa za kushiriki uwekezaji.
“Huduma hii ya Ununuzi na Uuzaji wa Hisa kupitia NMB Mkononi, ni matokeo ya Ubunifu na Ushirikiano baina ya NMB na DSE, uliounganisha mifumo ya NMB Mkononi na Hisa Kiganjani, bunifu na kazi kubwa iliyowezeshwa kwa juhudi za wataalamu wa TEHAMA kutoka pande zote mbili.
“Kupitia huduma hii tunayozindua leo, wateja wa NMB sasa wataweza kujisajili, kununua, kuuza hisa na kufanya malipo kupitia akaunti za NMB, kupata taarifa ya thamani ya uwekezaji wao, kuona bei za hisa zilizoorodheshwa DSE na kujua mwenendo wa Soko la Hisa la Dar es Salaam.
“Hili ni jukwaa linaloenda kuleta mapinduzi ya kweli katika ushiriki wa Watanzania kwenye Sekta ya Fedha, hususani Masoko ya Mitaji na Dhamana, lakini pia ni kielezo na uthibitisho wa dhamira ya dhati ya NMB kuwezesha ushirikishwaji wa kifedha kwa njia ya teknolojia,” alibainisha Bi. Zaipuna.
Akizindua huduma hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, alizipongeza NMB na DSE kwa ubunifu wa kiwango cha juu, unaoenda kuisadia Serikali ya Tanzania chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika maeneo makuu manne muhimu kiuchumi.
Aliyataja maeneo hayo aliyosema yamo katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo, kuwa ni pamoja na Kuimarisha Upatikanaji wa Huduma kwa Wananchi, Kusaidia Kubadili Mitazamo ya Wananchi, Kuelimish Jamii Juu ya Uwekezaji na Kuchagiza Ushirikiano kwa Taasisi za Ndani.
“Hili linalofanyika hapa ni tukio zuri na la maana sana, pongezi kwa NMB na DSE kwa huduma hii, kwetu sisi kama Serikali, hili ni jambo kubwa, muhimu na la maana sana linaloenda kutusaidia katika maeneo makuu manne ambayo ni muhimu kwa ustawi na ukuaji wa kiuchumi.
“Moja, huduma hii inaenda kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi, Serikali na Chama Tawala tunayo Mpango wa Maendeleo wa Taifa, ambao unataka ifikapo mwaka 2030, huduma zote za Kiserikali zimfikie mwananchi popote alipo, hili mnalozindua leo, mmetutangulia sana.
“Pili, mnaenda kusaidia kubadili mitazamo ya wananchi walio wengi. DSE ni kongwe, ilipoanza ilikuwa ngumu kumwambia Mtanzania anunue Hisa, sasa hii huduma inaenda kubadili mitazamo ya Watanzania juu ya Hisa, kwamba Utajiri sio tu kuwa na magari, majumba na viwanda, bali hata Hisa ni Utajiri pia.
“Pia katika eneo la tatu, huduma hii itakuza uelewa katika suala zima la uwekezaji. Kwa kweli huduma hii inaenda kuchochea uwekezaji miongoni mwa Watanzania. Inaenda kubadili mitazamo hasi juu ya uwekezaji kwamba sio kwa ajili ya wageni tu, bali hata wazawa wanapaswa na wanaweza kuwekeza.
“Ili uchumi ukue, watu wanahitaji kuwekeza na hatua ya kwanza ni uwekaji akiba, ili akiba izae, ndio linapokuja suala na ununuzi wa hisa, ambao unafaida kubwa. Eneo la nne ni ushirikiano mliokuja nao NMB na DSE. Ni taasisi za ndani zenye mafanikio na mnapokuja na aina hii ya ushirikiano, mnachagiza wengine,” alibainisha Profesa Kitila.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa DSE, Peter Nalitolela, alisema wao wanajisikia fahari sio tu kwa kuwa sehemu ya mashirikiano ya muda mrefu na NMB, bali ufanikishaji wa uzinduzi wa huduma bora ya kidijitali inayoenda kutanua wigo wa ushiriki wa Watanzania katika masuala mazima ya uwekezaji kwa njia ya hisa.
“NMB ni taasii inayoaminika, kinara wa ushirikiashaji jamii katika Huduma Jumuishi za Kifedha kwa Watanzania wa kadfa zote, ushirikiano huu na huduma hii ni uthibitisho kuwa taasisi hizi mbili zina dhamira ya dhati ya kukuza maslahi na ustawi wa wananchi.
“Wito wetu kwa umma hasa vijana, wawekeze sio kwa sababu wana pesa nyingi, bali kwa sababu wanahitaji kuwa na kesho iliyo bora na sisi kwa upande wetu, tunapambana kuondoa dhana hasi kuwa uwekezaji ni lazima uwe na mabilioni ya fedha, bali kwa kiasi chochote unaweza kuanza nacho uwekezaji,” alisema Nalitolela.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utafiti, Sera na Mipango wa Soko la Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Alfred Mkombo, akimwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, Nicodemus Mkama, aliitaja huduma hiyo kuwa ni hatua muhimu katika Sekta ya Fedha, hasa Soko la Mitaji na Dhamana nchini.
“Sisi CMSA tukiwa wasimamizi wa mitaji, tuna jukumu la kusimamia huduma zote za Masoko ya Mitaji, tunapongeza jitihada hizi za NMB na DSE kwa sababu ubunifu wao unaenda kutanua wigo wa Masoko ya Mitaji kuyafikia makundi yaliyoachwa nyuma katika hili.
“Hudum hii inayozinduliwa leo inaenda kuwa chachu ya wananchi wote kushiriki katika fursa za uwekezaji mijini na vijijini, hasa ukizingatia kuwa NMB Mkononi ina mtandao mpana unaojumuiosha wateja zaidi ya milioni 7 wa kada tofauti kote nchini.
“Tunazipongeza Bodi za NMB na DSE kwa ushirikiano huu unaozinda huduma hii iliyokidhi mahitaji na matakwa ya kikanuni ya CMSA,” alisisitiza Mkombo mbele ya waalikwa wa hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na Msajili wa Baraza la Soko la Mitaji na Dhamana, Martin Kolikoli.
No comments:
Post a Comment