
Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeelezea dhamira yake ya kuendelea
kushirikiana na wafanyabishara wadogo, wa kati na wakubwa kupitia huduma zake
mbalimbali za kibenki ili kuchochea ukuaji wa uchumi na mchango wa wadau hao
katika kufanikisha agenda ya Uchumi wa Buluu na uwezeshaji wa maendeleo
visiwani Zanzibar.
Dhamira hiyo imesisitizwa na Meneja wa benki ya NBC tawi la Zanzibar, Bw
Abdul Karim Mkila wakati akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa benki
hiyo Bw Theobald Sabi, kwenye hafla fupi ya Uzinduzi wa Jukwaa la Kimataifa la
Wakuu wa Mashirika na Kampuni visiwani Zanzibar linalofahamika kama ‘The
Tanzanite CEO Roundtable, Zanzibar Chapter’ iliyofanyika visiwani humo jana
jioni.
Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Mudrik Ramadhan Soraga
aliongoza uzinduzi wa jukwaa hilo, hafla iliyohudhuriwa pia na Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais (Kazi, Uchumi na Uwekezaji) Zanzibar, Sharif Ali Sharif.
Jukwaa hilo liliwakutanisha pamoja viongozi wa kampuni na mashirika kutoka
Tanzania, Kenya, Afrika Kusini, Mauritius na mataifa jirani likiwa na lengo la
kuimarisha uchumi wa buluu na kuwawezesha wafanyabiashara wa ndani. Benki ya
NBC ilikuwa miongoni mwa wadhamini muhimu wa jukwaa hilo.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Bw Mkila alibainisha umuhimu, nia na mchango
wa benki hiyo katika kushirikiana na wafanyabiashara pamoja na wadau mbalimbali
visiwani humo ili kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia huduma zake mbalimbali
zilizobuniwa mahususi kwa ajili yao ikiwemo mikopo na huduma za bima.
"Kimsingi ni kwamba NBC tumejizatiti kushirikiana na wadau wote katika
maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Jukumu letu ni kuhakikisha tunawawezesha
wafanyabiashara wadogo, wa kati, na wakubwa kwa kuwapatia huduma bora za
kibenki, mikopo na bima, ili waweze kufanya biashara zao kwa ufanisi
zaidi," alisema Bw. Mkila.
Aidha, aliongeza kuwa benki hiyo itaendelea kuwa mstari wa mbele katika
kuwezesha maendeleo ya kiuchumi kwa kuleta ushirikishwaji wa kifedha kwa
wafanyabiashara wa sekta zote.
Mbali na wakuu wa kampuni na mashirika, jukwaa hilo lililokuwa na kaulimbiu
‘’Kuimarisha Biashara za Ndani na Kujenga Uchumi Imara wa Buluu Zanzibar,” pia
liliwakutanisha wadau wengine wa biashara na uchumi wakiwemo wawekezaji.
Washiriki walipata wasaa muhimu wa kubadilishana mawazo, uzoefu, na mbinu za
kukuza biashara na fursa za uwekezaji visiwani Zanzibar.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri Soraga, alitoa wito kwa washiriki
kuendelea kushirikiana kwa ukaribu zaidi ili kukuza uchumi wa visiwa hivyo
hususani kupitia katika sekta za utalii, biashara, uvuvi na ujenzi wa makazi.
"Tukio hili ni nafasi adimu kwa wafanyabiashara, wakuu wa taasisi, na
wadau mbalimbali kukutana na kujadili kwa kina masuala muhimu kuhusu uwekezaji
na ukuaji wa uchumi. Serikali pia tunalitegemea jukwaa hili kama moja ya namna
bora zaidi katika kutusaidia kwa kutupatia ushauri kwenye masuala mbalimbali ya
kiuchumi ili kuleta maendeleo endelevu na jumuishi," alisema Waziri
Soraga.
Kwa upande wake Waziri Sharif, alisisitiza umuhimu wa wakuu wa makampuni
kukutana mara kwa mara ili kujadili fursa na changamoto zinazokabili sekta
mbalimbali za kiuchumi kwa kuwa mijadala na maoni yao kwa kiasi kikubwa
yatasaidia kuimarisha mazingira ya uwekezaji na kukuza uchumi wa Zanzibar
hususani kupitia agenda ya uchumi wa buluu.
“Kwa ujumla uzinduzi wa jukwaa hili la The Tanzanite CEO Roundtable, Zanzibar Chapter unatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo huku ukisaidia kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika sekta za uwekezaji na biashara, na kuleta mchango mkubwa kwa ustawi wa uchumi wa Zanzibar.’’ alisema




No comments:
Post a Comment