..........................
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam, Julai 4, 2024: Jumla ya washindi 60 wa mbio za NBC Dodoma
Marathon msimu huu wanatarajiwa kuondoka na zawadi zenye jumla ya thamani ya sh
milioni 82 pamoja na medali, imefahamika.
Mbio hizo zenye hadhi ya kimataifa zinatarajiwa kufanyika Julai 28, mwaka
huu kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma zikiwa na lengo la kukusanya fedha
ili kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi na kutoa ufadhili
wa elimu kwa wakunga ili kuboresha afya ya mama wa mtoto.
Hafla ya utambulisho wa zawadi hizo imefanyika jijini Dar es Salaam
ikihusisha maofisa kutoka benki ya NBC ambayo ndio inaratibu mbio hizo na wadau
wa mbalimbali wa mchezo huo wakiwemo waandishi wa habari tukio lililoshuhudiwa
na maelfu ya watazamaji kupitia vyombo mbalimbali vya habari vilivyokuwa
vikionesha mbashara tukio hilo lenye mvuto wa aina yake.
Wakifafanua kuhusu zawadi hizo Meneja Mahusiano ya Umma na Mawasiliano wa
benki ya NBC Bi. Brendansia Kileo na Meneja wa Biashara ya Kadi wa benki hiyo
Bi. Esnat Holella walisema viwango vya zawadi hizo vimeongezwa zaidi msimu wa
mwaka huu ikiwa ni muendelezo wa jitihada za benki hiyo katika kuongeza hadhi
ya mbio hizo kila mwaka.
Zaidi ongezeko hilo la viwango vya zawadi linatwaja kuwa linalenga
kuchochea ushiriki zaidi wa wanariadha wengi wakiwemo wa kimataifa, hatua
ambayo inalenga kuongeza ushindani zaidi kwa washiriki.
“Hivyo basi taarifa njema kwa washiriki wa NBC Dodoma Marathon mwaka huu ni
kwamba pamoja na medali kwa washiriki wote wa mbio hizi, washindi wa kwanza wa
mbio za kilomita 42 kwa wanaume na wanawake watajinyakulia Shilingi Milioni
11.5 kila mmoja, shilingi Milioni 5 kwa washindi wa pili, Shilingi Milioni 2.5
kwa washindi wa tatu, Shilingi Milioni 1.5 kwa washindi wanne na Shilingi
Milioni 1 kwa washindi wa tano, huku washindi wa sita hadi kumi nao pia
wakiibuka zawadi za na pesa taslimu.’’ Alisema Bi. Kileo.
Kwa upande wa mbio za Kilomita 21, Bi. Kileo alisema pamoja na medali
washindi wa kwanza kwa wanaume na wanawake watajinyakulia Shilingi Milioni 5.5
kila mmoja, Shilingi Milioni 2.5 kwa washindi wa pili, Shilingi Milioni 1.25
kwa washindi wa tatu, Shilingi 750,000 kwa washindi wanne na Shilingi 600,000
kwa washindi wa tano huku pia washindi wa sita hadi wa kumi wakiibuka na zawadi
za pesa taslimu kila mmoja.
“Mbio za kilomita 10 washindi wa kwanza wanaume na wanawake watajinyakulia
Shilingi Milioni 2.5 kila mmoja, Shilingi Milioni 1.5 kwa washindi wa pili,
Shilingi 750,000 kwa washindi wa tatu, Shilingi 500,000 kwa washindi wanne na
Shilingi 400,000 kwa washindi wa tano, huku washindi wa sita hadi kumi nao pia
wakiibuka zawadi za na pesa taslimu.’’ Aliongeza Bi. Kileo.
Aidha, Bi. Kileo aliongeza kuwa vifaa maalumu vitakavyotumiwa na washiriki
wa mbio hizo zikiwemo jezi vinatarajiwa kutolewa kwa washikiri katikati ya
mwezi huu huku akiendelea kutoa wito kwa jamii kuendelea kujisajili kupitia
tovuti ya www.events.nbc.co.tz na
kuchangia kiasi cha Shilingi 35,000 kwa usajili wa washiriki mmoja mmoja au
Shilingi 25,000 kwa usajili wa kikundi chenye idadi ya watu wanaozidi 25 ili
kuunga mkono agenda kuu ya mbio hizo.
Kwa upande wake Bi. Holella aliwashukuru wadau mbalimbali wanaoendelea
kujitokeza kushiriki maandalizi ya mbio hizo yakiwemo mashirika na kampuni
mbali mbali wakiwemo Sanlam Insurance ambao ni wafadhili wakuu wa mbio hizo
huku wadau wengine wakiwa ni Jubilee Allianz General Insurance, Wasafi Media,
Garda World, Metropolitan, SGA,SBC, Benki za CRDB na NMB, Computech Solutions
na Hans-Paul.
“Aidha kupitia ushirikiano wetu na Shirika la Reli Tanzania (TRC)
tunatarajia kwamba washiriki zaidi ya 1,000 watasafiri kutoka jijini Dar es
Salaam hadi Dodoma na kurudi kwa kutumia treni ya kisasa ya mwendokasi (SGR) ya
shirika hilo hatua ambayo inatarajiwa kuongeza radha zaidi ya mbio hizi msimu
huu wa tano,’’ alisema.
Utoaji wa zawadi zenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 80 kwa washindi
60 kuinaifanya mbio hiyo kuwa ndio mbio ya kwanza hapa nchini kutoa kiwango cha
zawadi kwa washindi wengi zaidi.
No comments:
Post a Comment