
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Afya iendelee kuwahamasisha
wananchi wabadili mitindo ya maisha ili kuepuka tabia zembe zinazochochea
ongezeko la magonjwa yasiyoambukizwa.
“Wizara ya Afya iendelee kushirikiana na wadau kuhamasisha Watanzania
kubadili mwenendo wa maisha kwa kuepuka tabia zembe zinazochochea ongezeko la
magonjwa yasiyoambukizwa. Tuendelee kuzingatia mazoezi ili kuimarisha afya zetu
na kuipunguzia Serikali mzigo wa kugharamia tiba ya magonjwa yasiyoambukizwa,”
amesema.
Akizungumza na viongozi, wananchi na wadau mbalimbali walioshiriki mbio za
NBC Dodoma Marathon za mwaka 2024 kabla ya kutoa tuzo na zawadi kwenye uwanja
wa Jamhuri, jijini Dodoma, leo (Jumapili, Julai 28, 2024), Waziri Mkuu amesema
takwimu za Wizara ya Afya zinaonesha kuwa idadi ya watu wenye magonjwa
yasiyoambukiza imeongezeka.
Amesema magonjwa yasiyoambukiza ambayo yanaongoza nchini ni pamoja na
kisukari, moyo, figo na afya ya akili na akatumia fursa hiyo kuwapongeza
wananchi walioshiriki mbio za hisani za NBC Dodoma Marathon za mwaka 2024.
“Kujitokeza kwenu kwa wingi leo, maana yake ni kwamba mmetambua kuwa kukaa
bwete ni kukaribisha magonjwa yasiyoambukiza,” amesisitiza.
Waziri Mkuu pia ameitaka Benki ya NBC iendelee kuweka mikakati ya
kuhakikisha mashindano hayo yanakuwa endelevu na yanaendelea kugusa maisha ya
Watanzania wengi zaidi.
Vilevile, amezitaka taasisi na asasi zisizo za Serikali zijitokeze kuunga
mkono jitihada za Serikali kwa kuandaa matukio kama hayo ili wananchi waanze
kuzoea kufanya mazoezi. “Tulishatoa maelekezo kwa Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na
Wilaya ili wawakusanye wananchi na kufanya mazoezi kama hivi,” amesema.
Amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha ustawi
na afya ya mtoto zikiwemo kutekeleza Mpango wa Mama Samia Mentorship ambao ni
mahsusi kwa utoaji mafunzo ya muda mfupi kazini kwa madaktari bingwa na
wakunga. “Hadi kufikia Juni 2024, halmashauri 184 zilishafikiwa na mpango huo
na idadi ya wanufaika ni watumishi 4,796,” amesema.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis
Mwinjuma alisema benki ya NBC ni wadau wakubwa katika sekta ya michezo kwa
kudhamini ligi ya soka ya Tanzania yaani NBC Premier League, kamati ya hamasa
inayochangia timu za Taifa na pia ni wadau wakubwa katika mfuko wa utamaduni
wenye lengo la kukopesha miradi ya kazi za sanaa nchini. Pia wanaendesha
marathon ambayo fedha zake hutumika kuchangia huduma za afya.
Amesema kuwa mbali na mbio hizo kutumika kuimarisha afya na kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza, pia zinatumika kama sehemu ya kuibua vipaji kwa wanamichezo hasa wanariadha ambao wamekuwa wakitumika katika michezo mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.
Mapema, akitoa taarifa kuhusu mbio hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC,
Theobald Sabi, alisema hii ni mara ya tano kwa mbio hizo kufanyika Dodoma huku
lengo likiwa ni kutangaza utalii wa Dodoma.
Alisema kwa mara ya kwanza mbio hizo zilifanyika Novemba 11, 2020 zikiwa na
washiriki 1,944 na waliweza kukusanya sh. milioni 100 lakini mwaka huu zimeweza
kupata washiriki 8,000 ambapo wameweza kukusanya sh. milioni 300.
Amesema makusanyo ya mwaka huu yatatumika kwenye ufadhili wa masomo kwa
wanafunzi wa taaluma ya ukunga kwa kushirikiana na Taasisi ya Benjamin Mkapa;
pia watasaidia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake
ambayo itakabidhiwa kwa taasisi ya Saratani ya Ocean Road.
“Pia fedha nyingine itatumika kuchangia ujenzi wa chumba cha upasuaji
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,” alisema.
Washiriki wa mbio hizo walikuwa ni wa km.5, km.10, km.21 na km.42
No comments:
Post a Comment