WIZARA YA FEDHA YASHAURIWA KUWA NA MPANGO ENDELEVU WA UTOAJI ELIMU YA FEDHA - UMOJA BANKING BLOG

Breaking

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, 25 June 2024

WIZARA YA FEDHA YASHAURIWA KUWA NA MPANGO ENDELEVU WA UTOAJI ELIMU YA FEDHA

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, mkoani Tabora, Bw. Seleman Mohamed Pandawe, akizungumza na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha ambayo ilifika ofisini kwake kujitambulisha na kuelezea njia watakazo tumia kufikisha elimu ya huduma ndogo za fedha katika Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge mkoani Tabora, Bw. Seleman Mohamed Pandawe (katikati) akipokea kitabu chenye mada mbalimbali ikiwemo uwekezaji, akiba na mikopo kitakachotumika kutoa elimu ya fedha kwa Wananchi wa Wilaya hiyo kutoka kwa Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha, Bi. Limi Bulugu (kushoto) na Afisa Uhusiano na Elimu kwa Umma Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bi. Stella John.
Baadhi ya Wananchi wa Wilaya ya Sikonge, mkoani Tabora, wakisoma vipeperushi vyenye mada mbalimbali ikiwemo mikopo, akiba na uwekezaji zilizotolewa na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha ambayo ipo mkoani Tabora kutoa elimu ya fedha kwa Wananchi wa makundi mbalimbali wakiwemo Watumishi, Wafanyabiashara na Wajasiriamali.
Baadhi ya Wananchi wa Wilaya ya Sikonge, mkoani Tabora, wakifuatilia mada mbalimbali zilizotolewa na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha ambayo ipo mkoani Tabora kutoa elimu ya fedha kwa Wananchi wa makundi mbalimbali wakiwemo Watumishi, Wafanyabiashara na Wajasiriamali.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WF, Tabora)
------------------

NA: JOSEPHINE MAJULA, WF, TABORA

 

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, mkoani Tabora, Bw. Seleman Mohamed Pandawe, ameishauri Wizara ya Fedha kuwa na mpango endelevu na wa muda mrefu wa utoaji elimu ya fedha kwa wananchi kwa kuwa elimu hiyo ni muhimu na ina mchango katika ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

 

Bw. Pandawe, ametoa ushauri huo alipokutana na Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha ambayo ilifika Wilayani mwake kutoa elimu ya fedha kwa Wananchi ili waweze kutumia fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya fedha na kujikomboa kiuchumi.

 

“Uhitaji wa elimu ya fedha bado ni mkubwa sana, sisi wenyewe ni mashahidi ndugu na jamaa zetu waliopo maeneo mbalimbali hususan vijijini hawana elimu ya utunzaji fedha, wengi wao wanachimbia chini fedha hadi zinaliwa na mchwa zinakua hazifai tena kwa matumizi”, alisema Bw. Pandawe.

 

Alisema kuwa wilayani kwake Wananchi wanafanya shughuli mbalimbali za kiuchumi, lakini fedha wanazopata na maisha yao hayaendani kutokana na kutokuwa na elimu ya masuala ya fedha ikiwa ni pamoja na elimu ya nidhamu ya matumizi binafsi, kutumia fedha zisizozidi kipato chao, na kuwa na mazoea ya kujiwekea akiba.

 

Bw. Pandawe aliipongeza Wizara ya Fedha kwa kuwafikia Wananchi wa makundi mbalimbali kuwapa elimu muhimu ya fedha, na kuongeza kuwa wanachi wengi wana vipato lakini hawana uelewa ya namna bora ya kutumia fedha.

 

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Ipole, Bw. Deus Evalist, aliipongeza Timu ya Wataalamu ya Wizara ya Fedha kuwafikia na kuwapa elimu hiyo muhimu itakayokwenda kubadilisha mfumo wao wa maisha katika matumizi ya fedha bila kuwa na bajeti.

 

 Kwa upande wake Afisa Mtendaji Kata ya Ipole, Bi. Clementina Kadiko, aliahidi kushirikiana na viongozi wenzake ngazi ya kata kuhakikisha kila mwananchi anapata elimu hiyo muhimu ili waweze kuwa na mipango yenye tija katika matumizi ya fedha zao na kujikwamua kiuchumi.

 

Naye Afisa Uhusiano na Elimu kwa Umma kutoka Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Bi. Stella John, aliwashukuru wananchi wa mkoa wa Tabora kwa kushiriki kikamilifu semina zilizotolewa.

 

“Wananchi wameonesha ushirikiano mkubwa, kuna waliouliza maswali, kuna waliojibu lakini pia kuna waliotoa maoni na ushauri ambao tumeuchukua na tutauzingatia awamu nyingine”alisema Bi. Stella John.

 

Wizara ya Fedha inaendelea na zoezi la utoaji elimu kwa wananchi kuhusu huduma ndogo za fedha ikiwa ni Utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa mwaka 2021/2022 hadi 2029/2030.

 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad

Pages